Monday, March 24, 2014

WAJUMBE BUNGE LA KATIBA WATAKIWA KUACHA UBINAFSI, UCHOYO...

Kingunge Ngombale Mwiru akichangia katika semina hiyo.
Kutokana na kuongezeka mivutano na mpasuko miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,  imeshauriwa njia pekee ya kunusuru mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya ni wajumbe kuacha ubinafsi, uchoyo na misimamo ya kisiasa badala yake wajenge maridhiano.

Mwito huo ulitolewa jana na mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally wakati wakitoa mada kwenye semina ya waandishi wa habari za Bunge mjini hapa.
Mada ya Kingunge ilihusu mtazamo wake kuhusu mapendekezo ya Tume kuhusu  Muungano wakati ya Bashiru ilihusu ‘Katiba mpya kwa mustakabali wa taifa letu.’
Katika mada zao, wote walikiri mazingira ya kisiasa kwa sasa siyo rafiki, kama ilivyokuwa wakati Tume ikikusanya maoni.
Walisema pamoja na hali hiyo,  wajumbe wa Bunge hilo wanapaswa kujenga msingi wa maridhiano kwa sababu kutofanya hivyo, kuna madhara makubwa ya kisiasa, siyo tu kwa wao, bali  pia kwa taifa zima.
Kingunge katika mada yake, alisema iwapo wajumbe wataendelea kukumbatia maslahi ya vyama vyao, Bunge hilo halitafika popote na matokeo yake itakuwa ni kuvunjika.
 Hata hivyo, Kingunge alisema anaamini licha ya tofauti hizo ndani ya Bunge Maalumu, zipo  busara nyingi ambazo watatumia kupata mwafaka.
“Tutaunganisha mawazo tofauti haya kama tulivyofanya kwa Zanzibar, katika hili la Katiba linawezekana ili mradi wajumbe waache uchoyo,” alisema Kingunge.
Uchoyo aliosema Kingunge ni upande wa Chama Cha Mapinduzi, kuona kwamba wapinzani wanataka kuandaa mazingira ya kuwanyang’anya madaraka hivyo wanaweza kupambana kuhakikisha ajenda zao pekee  ndizo zinapita.
Lakini, alisema wapinzani pia wanaona kwamba njia pekee ya kudhoofisha CCM ni nchi kuwa na serikali tatu, badala ya mbili na hivyo wakang’ang’ania suala hilo bila kuhitaji majadiliano.
“Misimamo  ya pande hizi mbili ikishikiliwa na wajumbe, ni wazi kuwa hatuwezi kufika popote, lakini tufanye kama tulivyofanya Zanzibar ili muafaka wa Katiba uweze kupatikana,” alisema Kingunge.
Katika mazungumzo yake, Kingunge alisisitiza kuwa wajumbe wanatakiwa wawapatie wananchi Katiba nzuri yenye mambo mapya ambayo hayakuwemo kwenye hotuba ya awali. Pia alisisitiza masuala yanayohusu wananchi ni lazima yaingizwe.
Kwa upande wake, Bashiru Ally alisema mnyukano ndani ya Bunge Maalumu, haukwepeki; isipokuwa alishauri ni vyema wajumbe wajenge maridhiano  kuipatia nchi Katiba nzuri.
Alisema wajumbe wajifunze kwa Tume ya Marekebisho ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba kwamba licha ya kuwa walitofautiana, waliweka pembeni  tofauti za itikadi zao na kuweka msingi wa maridhiano.
“Maridhiano hayakwepeki, licha ya kuwa watavutana serikali mbili au tatu, lakini mwisho wa siku wajenge maridhiano,” alisema Bashiru na kuwataka wajumbe hao kutumia taarifa zote za Tume na hotuba ya Rais, kama nyenzo ya utendaji wao.
Alionya, iwapo makundi hayo yatakumbatia ama hotuba ya Rais peke yake au ya Jaji Warioba, hawawezi kufikia muafaka wa kutunga Katiba mpya. Alishauri hotuba zote mbili na taarifa za tafiti za Tume zisomwe kwa pamoja.
Alisema suala la muundo wa Muungano ni nyeti, linalohitaji kupata maridhiano ya pamoja. Alishauri wanaotaka serikali tatu, waje na hoja kushawishi wenzao kwamba serikali hiyo inahitaji kuwa madhubuti kuliko serikali za nchi washirika.
Kwa upande wake, Dk Ayoub Rioba,  katika mada yake kwa vyombo vya habari na mchakato wa Bunge la Katiba, alishauri waandishi wa habari kuhakikisha taarifa juu ya yote yanayoendelea katika Bunge Maalumu, zinafikia wananchi haraka.
Aidha alishauri  taarifa ziwe zenye manufaa kwa wananchi  na ziwe sahihi, katila lugha fasaha na yenye staha  kuepuka upotoshaji.
Waziri  wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara alitaka waandishi wa habari, kujituma na kuepuka kutumika kubomoa jamii na kubeba masuala yasiyojenga na kuyafanya ndio wananchi wanayahitaji kuyajua na kuacha yale yanayochochea kupatikana kwa Katiba mpya.
Dk Mukangara  alisema suala la kutengeneza Katiba ya nchi, siyo jambo rahisi. Aliomba waandishi wa habari wawe watulivu, waache ushabiki wa aina yoyote na uwezekano wa kuwa wakala wa mtu au watu na kutumika kwa namna yoyote, kuleta mkanganyiko kwa wananchi.
 Alisema Tanzania inahitaji wanahabari wenye uzalendo, maadili na weledi na wawajibikaji katika nafasi yao ya kufikia wananchi.
 Alisema taifa linahitaji wanahabari, wenye kuhakikisha masuala yenye maana kwa maendeleo ya wananchi na nchi yanafikia walengwa, ambao ni wananchi.
Bunge Maalumu la Katiba  linaendelea leo na vikao vyake; huku miongoni mwa shughuli zake, zikiwa ni  kuundwa kwa kamati 15, zikiwemo  12 za kudumu.
Pamoja na uundaji wa kamati, wiki hii inatarajiwa uamuzi juu ya kura ya siri au ya wazi katika kupitisha masuala mbalimbali bungeni, utapatiwa ufumbuzi.
Kamati hiyo zikishaundwa zitatakiwa kuchagua mwenyekiti na makamu mwenyekiti ambao ndio watakuwa na jukumu la kuziongoza kujadili sura mbalimbali za rasimu ya Katiba.
Kwa upande wa kamati zisizo za kudumu  ni Kamati ya Uongozi , Kamati ya Kanuni na Kamati ya Maridhiano.
 Kamati zikishakutana kazi yake ni kujadili sura mbili za rasimu hiyo na kutoa taarifa mbili, moja ikiwa ni taarifa ya wengi na nyingine  ya wachache, ambazo zote zitawasilishwa bungeni na mwenyekiti na mjumbe mwingine atakayewasilisha maoni ya wachache.
Ili kupata maoni ya wengi na wachache kwa kila sura, ni wazi lazima kura ipigwe. Hivyo kitendawili cha kura gani itatumika katika kamati hizo ni lazima kipatiwe ufumbuzi kabla ya kuanza kwa kamati hizo.
 Kura hizo zitahusu pia pande za Muungano, ambako ndani ya kamati na ndani ya Bunge Maalum ni lazima kura ziwe theluthi mbili kwa Bara na theluthi mbili kwa Zanzibar ili jambo liweze kupitishwa.
Kamati ya Kanuni ilipendekeza kura ya siri itumike katika uamuzi, lakini wajumbe walitofautiana kutokana na kuwepo kundi linalotaka kura iwe ya wazi.
Wanaotetea kura ya siri wanasema kura ni dhamira ya mtu inavyomtuma. Pia wanasema yako mambo ambayo wanaweza kupiga kinyume na wananchi wa jimbo lake jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wao.
 Lakini wanaotetea kura ya wazi wanasema kwa mambo makubwa kama hilo la kutunga Katiba, ni lazima wajumbe wawe wazi na wananchi wajue amepiga kura upande upi. Wanasema kwamba kupiga kura ya wazi kutasaidia kila mjumbe kujua msimamo wake.
Katika mvutano huo, wajumbe wengi wanaotokana na CCM, ndiyo wanaotaka kura ya wazi huku wanaotoka vyama vya upinzani wanataka kura ya siri.
Kiini cha mvutano huo, ni msimamo wa makundi ndani ya Bunge hususani kuhusu suala la muundo wa Muungano; kwa maana ya serikali mbili na wa serikali tatu.

No comments: