Friday, March 21, 2014

RAIS KIKWETE KUNGURUMA BUNGE LA KATIBA LEO SAA 10 JIONI...

Rais Jakaya Kikwete, leo anatarajiwa kuhutubia Bunge Maalumu la Katiba na hotuba yake kurushwa moja kwa moja na Televisheni ya Shirika la Utangazaji (TBC). 

Hotuba hiyo ya Rais, imekuwa ikisubiriwa kwa hamu na Watanzania kutoa dira kwa wajumbe wa Bunge hilo Maalumu la Katiba, wakati watakapokuwa wakiandika Katiba mpya. Kwa mujibu wa Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahya Khamis Hamad, Rais atahutubia Bunge saa 10 jioni na wageni waalikwa watatakiwa kuwa wameketi katika maeneo yao saa tisa alasiri.
Hamad alisema ratiba ya shughuli hiyo itaanza na kikao cha Bunge saa 9.10 na baadaye kikao hicho kitaahirishwa saa 9.20 kwa ajili ya kumpokea Rais Kikwete.
Wageni mashuhuriHamad alisema Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, amewaalika wageni mbalimbali kushuhudia tukio hilo muhimu la kitaifa, wakiwemo viongozi wa kitaifa na watendaji wakuu kutoka pande zote za Muungano.
Miongoni mwa wageni mashuhuri watakaokuwepo, ni pamoja na mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, mjane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mama Fatma Karume, marais wastaafu Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na mawaziri wakuu wastaafu.
Wengine ambao wamealikwa kuhudhuria tukio hilo ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, wajumbe wenzake na makamishna wote wa Tume hiyo.
Pia watakuwepo viongozi wengine wastaafu wa kitaifa ambao mawaziri wakuu wastaafu, Waziri Kiongozi mstaafu na maspika wa Bunge.
Wageni wengine walioalikwa ni kutoka taasisi za dini, taasisi zisizo za kiserikai, wawakilishi wa tasnia ya habari, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu na  taasisi za elimu ya juu.
Pia vipo vyama vya watu wenye ulemavu, vyama vyawafanyakazi, vyama vya wafugaji, vyama vya wavuvi na wakulima pamoja na wawakilishi kutoka sekta binafsi.  
Mara baada ya Rais kuwasili katika eneo la Bunge,  atapokewa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba na baadaye kwenda  katika jukwaa maalumu kupokea salamu za heshima na kukagua gwaride maalumu lililoandaliwa na Polisi.
Katibu wa Bunge alisema baada ya shughuli zote zitakazofanyika katika viwanja vya Bunge kumalizika, utaratibu umewekwa kwa viongozi kuingia bungeni kwa maandamano maalumu.
Maandamano hayo yatatanguliwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif  Sharif Hamad, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Gharib Mohammed Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Rais Kikwete ambaye atakuwa amefuatana na mwenyeji wake ambaye ni Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta.
Baada ya Rais kumaliza kuhutubia Bunge Maalum, wajumbe wote wa Bunge Maalum watapata fursa ya kupiga picha ya pamoja mbele ya jengo la Bunge.
Rais atalihutubia Bunge ili kutoa nafasi kwa Bunge hilo   kuendelea na mjadala baada ya Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Pili Jumanne wiki hii.

No comments: