Wednesday, March 26, 2014

RAIS KIKWETE AVUNJA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA...

Jaji Joseph Warioba.
Rais Jakaya Kikwete ameivunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba, baada ya tume hiyo kumaliza kazi iliyopewa na kukabidhi Rasimu ya Katiba kwa Bunge Maalumu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais aliunda tume  hiyo  kwa mujibu wa kifungu cha 5 na 6 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 kwa Tangazo la Serikali Na.110 la Mwaka 2012.
Majukumu ya tume hiyo yalikuwa ni pamoja na kukusanya maoni kwa wananchi na kuandaa rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kazi ambayo imefanywa na tayari imeshawasilishwa kwenye Bunge Maalumu ya Katiba.
Taarifa hiyo ilisema, kwa mujibu wa kifungu cha 31, cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 3, Rais amepewa mamlaka ya kuvunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya Rasimu ya Katiba kuwasilishwa Bungeni.
Na kwamba Machi 18, mwaka huu, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba aliwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu.
Hivyo kwa mujibu wa kifungu cha 31, cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais alivunja  rasmi tume hiyo Machi 19, mwaka huu kwa Tanganzo la Serikali namba. 81 la Machi 21, 2014.
Hivyo kwa tangazo hilo, shughuli zote za Tume ya Mabadiliko ya Katiba zimemalizika rasmi tarehe 19 Machi, 2014.
Mbali na majukumu hayo, tume hiyo pia ilikuwa na majukumu ya kuandaa na kuendesha programu za kuelimisha umma, kuitisha na kusimamia mikutano ya mabaraza ya katiba na kutathmini na kuchambua maoni ya wananchi.
Kadhalika kazi nyingine za tume zilikuwa ni kupitia na kuchambua michango, mawazo, maoni na taarifa pamoja na mapendekezo yaliyokusanywa na kufanyiwa tathmini siku za nyuma na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya kikatiba yanayohusu mamlaka ya wananchi.
Pia tume ilichapisha rasimu ya Katiba katika gazeti la Serikali na magazeti mengine ili kutoa fursa kwa wananchi kusoma na kutoa maoni zaidi kwa tume kupitia mabaraza ya Katiba na kisha kutayarisha na kuwasilisha ripoti kwa kila hadidu ya rejea.
Hata hivyo baada ya kukamilisha hayo yote tume hiyo ilitoa rasimu ya kwanza ya Katiba Juni mwaka 2013 na kisha Rasimu ya pili ilitolewa Desemba na kukabidhiwa kwa rais.
Kisha hatua ya mwisho ni rasimu hiyo kuwasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba ambalo muda wowote kuanzia hivi sasa litaanza kuijadili.
Katika rasimu ya Katiba mpya mambo yaliyoonekana kuleta gumzo ni suala la muundo wa Muungano, ambalo mapendekezo ya wananchi ni kuwa na miundo mitatu ya muungano.
Muundo wa kwanza ni serikali moja, muundo wa serikali mbili na muundo wa serikali tatu.
Ambapo tume imeshauri kuwepo kwa muundo wa serikali tatu, jambo ambalo rais ameshauri wajumbe wa bunge hilo kufanya maamuzi sahihi juu ya muundo wa serikali huku wakizingatia  manufaa na changamoto za kila muundo wa serikali zilizopendekezwa.
Tume hiyo ilikuwa na wajumbe 32, ilikuwa na jukumu la kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kupatikana kwa Katiba mpya.
Tume hiyo imefanya kazi kwa muda wa miezi takribani 23, na ilianza kufanya kazi rasmi Mei 2, mwaka 2012 baada ya wajumbe wake kuteuliwa Aprili 6, mwaka 2012 na kuapishwa rasmi Aprili 13, mwaka 2012.

No comments: