![]() |
| Rais Jakaya Kikwete akisisitiza jambo alipolihutubia Bunge la Katiba jana. |
Rais Jakaya Kikwete amesema muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba hautekelezeki na kusema kero za Muungano zinaweza kutatulika kwa kuendelea na serikali mbili.
Alisema hayo wakati wa hotuba yake kwa Bunge jana, hotuba ambayo inaonekana kama hotuba elekezi ikiwa inachambua kwa kina historia, athari na athira za matendo yaliyofanyika katika Muungano na rasimu ya Katiba .
Katika hotuba yake pamoja na kuwataka wajumbe kuamua wenyewe kwa kuwa makini amesema kwamba serikali tatu kutekelezeka kwake ni kugumu kutokana na muundo wenyewe na namna ya kujipatia mapato.
Rais Kikwete alisema kutotekelezeka kwake kunatokana na serikali hiyo ya tatu kutokuwa na mapato ya uhakika, kwani haina chombo cha kukusanya mapato na badala yake inategemea nchi washirika zikusanye mapato na kuipelekea.
Alisema serikali hiyo itakuwa itegemee hisani za nchi washirika na iwapo nchi moja itaondoa hisani zake serikali ya tatu itayumba na kusisitiza; “Kuna hatari wakati wowote serikali hiyo ya Muungano kusimama, lazima tutengeneze kitu thabiti na uwepo msingi imara.
“Serikali ya muungano ya tatu haina nyenzo wala uwezo kuhakikisha mapato yanawasilishwa. Kama tunataka kitu lazima tujipe muda tuhakikishe inasimama…rasimu inapendekeza kuweza kukopa, lakini serikali hiyo haina rasilimali na rasilimali zake ni jeshi na mizinga yake,polisi na magari yake ya washawasha, pingu na magereza yake.
“Nani hapo anakudhamini kwa rasilimali hizo? Serikali hiyo ya tatu haikopesheki labda Tanganyika iidhamini kwa sababu ina gesi, dhahabu, mtama, muhogo, mbuzi, ng’ombe na hapo asiye na kitu kinyama mwitu. Mtasema mimi si muumini wa serikali tatu, lakini hata hao waumini wa hiyo wanajua … Wabunge wekeni sawa jinsi hiyo serikali tatu itakavyokuwa, wekeni majibu ya kukwamua matatizo yakitokea.”
“Jiridhisheni hiyo serikali itaweza kusimama ila naona itakuwa tegemezi na egemezi kwa kuwa haina kipato na siku ikishindwa kuwalipa mishahara wanajeshi, watakuja kuwaondoa hao na mfumo wa kiafande hauna demokrasia, Katiba inafutwa na yeye hana sehemu ya kuwajibika, atasema anachukua madaraka kwa miaka mitano kuweka mambo sawa baadaye anavua gwanda anagombea urais…hayo ni maoni yangu yanaweza kutokuwa na msingi lakini watakaoamua tuwe na serikali tatu au mbili ni nyinyi na ndo itakuwa chetu lakini kama mnataka serikali tatu iwe itakayosimama si kutaka tu,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete aliyehutubia Bunge kwa saa mbili na dakika 40 alitahadharisha hisia za utaifa ya kutaka kuwe na serikali tatu italeta Uzanzibari na Utanganyika ambao zamani haukuwepo kwani asilimia 90 ya Watanzania wamezaliwa baada ya mwaka 1964 hivyo wanachojua ni Muungano na hawaijui Tanganyika.
“Mkishaitengeneza Tanganyika baadhi ya watu watakuwa wageni haitakuwa rahisi kama Jaji Warioba alivyosema watu wataweza kupiga kura popote na kugombea uongozi na wabaya wataingia hapohapo…msigeuze jambo dogo kuwa na serikali ya tatu, nimesoma sana mapendekezo ya Tume hayajaja majawabu ya uhakika na kama mnataka kila mtu aende kwake sawa lakini subirini wakati miye sipo.”
“Mwaka 2012 Zanzibar kulitokea kikundi kikachochea hisia za Uzanzibari mliona maduka ya wabara yalivyochomwa sasa ikitokea huku Tanganyika yatakuwa makubwa zaidi na yatakayotokea baada ya hapo tutayajutia,” alisema.
Alihoji hoja ya Jaji Warioba ya kutetea serikali tatu kwa kuhoji watu 351,000 na watu 47,000 ndiyo waliozungumzia muundo wa serikali ya Muungano na yachukuliwe kama maoni ya Watanzania wote. Hata hivyo aliwataka wajumbe wenyewe kulitafakari hilo.
Alisema changamoto zilizopo kwenye mfumo wa serikali mbili zinaweza kutatuliwa bila kuongezwa serikali tatu na hata Jaji Warioba kwenye ripoti yake amelieleza hilo kwa kuonesha faida nyingi za kuwepo serikali mbili.
Rais alisema ana matumaini kwa vile dhamira ni njema kuwa kero za Muungano zinaweza kumalizwa kwenye serikali mbili tofauti na Jaji Warioba aliyeonesha kukata tamaa na kufikia suluhisho la serikali tatu na kuonesha mkazo “tukikata tamaa linalofuata ni wacha tuzame, tugawane mbao”.
Aidha, aliwaeleza wajumbe hao kuwa wao ni viongozi na wana dhamana kuamua kwa niaba ya wananchi na watajutia maamuzi yao pindi wakiona machafuko na Muungano unakufa na hapo ndipo watakapoona sababu za waasisi wa Muungano kuamua serikali mbili na walichojenga kwenye Muungano wa miaka 50.
Aliwataka wajumbe hao wa Katiba kujipa muda wa kutafakari zaidi hasara na faida za Muungano wa serikali mbili na kutochoka kutafuta majawabu ya matatizo yaliyotokea kwenye muundo wa serikali mbili.
Aliwataka kuipa Tanzania hatma njema kwa kujadili na kufanya maamuzi kwa kuzingatia neno kwa neno, sentensi kwa sentesi, ibara kwa ibara, sura kwa sura na vifungu kwa vifungu.
Alisema ingawa vyama vya siasa vya wajumbe hao na makundi yao yamewapa misimamo yao si vibaya wakaifuata kama shabaha yake ni kujenga na kama ni kubomoa waachane nayo.
Hata hivyo, aliwaambia wazingatie umakini na si kila wanaloambiwa wanalichukua bila kulichuja ambapo aliwasisitizia “akili za kuambiwa changanya na zako”.
Rais Kikwete alisema si jambo jipya kwa Tanzania kudai serikali tatu lakini wakati wote imeshindikana na kuwataka safari hii jambo hilo limalizwe kwa kuwepo serikali tatu au serikali mbili ili watu wafanye kazi nyingine.
Suala la serikali tatu lilisababisha mwaka 1984 kuchafuka hali ya kisiasa na mwaka 1992 likapendekezwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali, mwaka 1993 hoja hiyo ikaletwa tena na kundi la wabunge waliojiita G55 mwaka 1998 ikapendekezwa tena na Jaji Robert Kisanga lakini wakati wote halikupita.
Mwanzoni mwa wiki hii, Jaji Warioba wakati anawasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba bungeni alieleza kuwa suluhisho la kero za Muungano kwa pande zote za Muungano ni kuundwa kwa serikali tatu na Zanzibar na Tanganyika zikiwa na mamlaka yake.
Wakitoa maoni nje ya Bunge mara baada ya Rais Kikwete kuhutubia Bunge walipongeza hotuba hiyo na miongoni mwao ni George Simbachawene aliyesema hotuba ya Rais Kikwete ni uthibitisho wa Watanzania wanachotaka na kwa kuzingatia alichosema itafanya Katiba mpya itakapopatikana idumu.
Naye Ismail Aden Rage alisema wataangalia maslahi ya nchi, kushindana kwa hoja na kuhakikisha wanawatengenezea wananchi Katiba ya umoja na muafaka kwa kuweka utaifa kwanza na kuongeza “ Tutaomba Mungu atuwezeshe tupunguze jazba na kuweka mbele maslahi ya nchi yetu”.
Nyambari Nyangwine alisema hotuba hiyo imefungua milango ya historia. Ametoa hotuba kwa ujasiri na waliokuwa na mawazo tofauti ya kutaka serikali tatu sasa wataungana na wenye msimamo wa serikali mbili. Alisema “tutaipigania kwanza Tanzania mengine baadaye”.

No comments:
Post a Comment