![]() |
| Mwenyekiti wa muda, Pandu Kificho akiingia bungeni. |
Eneo lingine ambalo ni moto kwa Bunge Maalumu ni juu ya utaratibu wa Bunge hilo kufanya uamuzi ambao rasimu inaelekeza kuwa ili hoja au ibara ipite ni lazima iungwe mkono na wajumbe theluthi mbili kutoka Bara na theluthi mbili kutoka Visiwani.
Kutokana na wajumbe hao wa kamati ya mashauriano kushindwa kuafikiana, Mwenyekiti wa muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Ameir Pandu Kificho alilazimika jana kuliweka suala hilo kiporo hadi hapo maafikiano yatakapofikiwa na kamati hiyo.
Suala la kura iwe ya siri au ya wazi katika kupitisha vifungu vya rasimu ya katiba limekuwa moto na juzi lilisababisha Bunge kuahirishwa siku nzima ili kutoa nafasi kwa kamati ya mashauriano kulijadili na hatimaye kufikia muafaka.
Lakini kwa kuwa taratibu zinawataka wajumbe wa kamati hiyo kupeleka taarifa kwenye vikao vyao vya chama, ilielezwa kuwa baada ya wajumbe hao kumaliza kikao juzi saa tatu usiku, kila mjumbe alilazimika kupeleka taarifa za kikao cha kamati hiyo ya mashauriano kwenye chama chake.
Kutokana na suala hilo kuwa gumu, ahadi ya Kificho kuwa utungaji wa kanuni kukamilika jana umeshindikana na hivyo suala hilo sasa linaenda hadi Jumatatu, hivyo kuchelewesha uchaguzi wa mwenyekiti na kuapa kwa wajumbe.
Kwa mambo yanavyokwenda ni wazi kuwa wiki ijayo rasimu ya Katiba pia inaweza isiwasilishwe na wala Rais Jakaya Kikwete anaweza asilifungue Bunge hilo, kwani kuapishwa kwa wajumbe hao kunaweza kuchukua siku tatu au nne.
Tathmini ya mwandishi wa habari hizi inaonesha kuwa wapinzani wanaunga mkono kura ya siri huku wajumbe 201 ambao ni wateule wa Rais ambao sio wanachama wa vyama wana misimamo ya kati na wako tayari kwa kura zote zitumike.
“Kuna vifungu kama vitano tu kwenye rasimu ya katiba ambavyo vinahitaji kura ya siri, vingine hata ikiwa kura ya wazi hakuna madhara,” alisema mjumbe mmoja.
Mvutano huo kwenye kura na maamuzi pia ulisababisha vikao vya Bunge ambavyo vilikuwa vifanyike jana asubuhi kuahirishwa hadi saa tisa alasiri. Lakini kikao hicho pia hakikuanza muda huo badala yake Kificho aliingia bungeni hapo saa 10.40 na kuwaomba radhi wajumbe kwa kuchelewa kuanza kikao hicho.
Kificho aliwaambia wajumbe hao alichelewa kwa vile kulikuwa na masuala muhimu ambayo walikuwa wanayafanya na kamati ya mashauriano kwa manufaa ya Bunge hilo. Alisema kamati hiyo iliamua kuwa kazi ya kupitisha kanuni 10 zilizobaki kufanyike nusu na suala la kura ya siri au wazi bado linatafutiwa ufumbuzi.
“Kamati imenishauri suala jema kuwa vifungu 37 na 38 tuviache ili kamati hiyo ya ushauri iendelee kunishauri vizuri zaidi,” alisema Kificho na kuongeza kuwa, “wameafikiana hivyo ili kamati hiyo iweze kushauriana zaidi na waje na kitu kizuri makusudi, ikiwa ni kuja na jambo lenye mashiko.”
Vifungu hivyo moto ni 37 kinachosema, “Bila kuathiri masharti ya sheria na kanuni hizi, utaratibu wa Bunge maalumu kufanya uamuzi utakuwa ni kwa mwenyekiti kulihoji Bunge maalum na kupata uamuzi wa Bunge maalum utakaotokana na wingi wa idadi ya wajumbe kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na kanuni hizo.
“Isipokuwa kwamba, ili ibara au rasimu ya katiba iweze kupitishwa katika Bunge maalum itahitaji kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge maalum kutoka Tanzania Bara na theluthi mibili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge maalum kutoka Tanzania Zanzibar.
“Iwapo jambo lolote linatahitaji kuamuliwa au kutekelezwa na Bunge maalum, basi jambo hilo halitahesabiwa kuwa limeamuliwa au limetekelezwa ipasavyo; ili mpaka liwe limeamuliwa au limetekelezwa na Bunge maalum kwa kuzingatia masharti na utaratibu uliowekwa na sheria pamoja na kanuni hizi.
“Kwa madhumuni ya kanuni hii, utaratibu utakaotumika kupata uamuzi baada ya mwenyekiti wa Bunge maalum kutoa swali la kulihoji Bunge maalum utakuwa ni kwa kuwa ya siri. Bila kuathiri masharti ya sheria na kanuni hizi, wakati wa kupata uamuzi wa Bunge maalum kuhusu kupitisha rasimu ya katiba, Bunge maalum litapiga kura ya siri ambayo kwa madhumuni ya kanuni hii itakuwa kura ya mwisho,” kinasema kifungu hicho.

No comments:
Post a Comment