Wednesday, March 19, 2014

MAHAKAMA YATUPILIA MBALI OMBI LA SHEKHE PONDA...

Shekhe Ponda Issa Ponda.
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali ombi la mapitio lililowasilishwa na Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shekhe Issa Ponda kwa kuwa limewasilishwa kinyume cha sheria.

Jaji Augustine Mwarija alitoa uamuzi huo jana baada ya kuridhika na hoja za pingamizi la awali lililowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kabla ombi hilo halijaanza kusikilizwa.
Katika ombi hilo, Shekhe Ponda aliiomba Mahakama ifanye mapitio ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, uliokataa kumfutia mashitaka ya kukiuka amri ya Mahakama.
Akitoa uamuzi, Jaji Mwarija alisema ombi hilo limewasilishwa kinyume na kifungu cha 372 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ambacho kinakataza maombi hayo kufanyiwa mapitio.
Alisema kifungu hicho kinasema, hairuhusiwi kuwasilisha ombi la mapitio ya amri yoyote ya awali au ya muda iliyotolewa katika Mahakama za chini isipokuwa kama uamuzi au amri hiyo inamaliza kesi ya jinai.
Aidha Jaji Mwarija alisema tafsiri iliyotolewa na Wakili wa Ponda, Nassoro Juma kuwa uamuzi au amri iliyotolewa kutokana na pingamizi la awali inamaliza kesi siyo sahihi, pia aliegemea katika kipengele kimoja cha kifungu hicho.
Alisema Shekhe Ponda anakabiliwa na kesi ya jinai yenye mashitaka matatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro na uamuzi uliotolewa katika pingamizi la awali haukumaliza mashitaka yake.
Aliongeza kuwa kifungu husika, hakihusiani na kumaliza pingamizi la awali bali kumaliza kesi yote, lakini pingamizi la awali linaweza  kumaliza kesi endapo pande zote mbili zitakubaliana kesi iishe.
Alisema kutokana na sababu hizo Mahakama inakubali hoja za pingamizi la awali na kulitupilia mbali ombi hilo kwa kuwa liliwasilishwa kinyume cha sheria ambayo hairuhusu maombi hayo kuletwa isipokuwa kama yatakuwa yanamaliza kesi.
Ponda anadaiwa kukiuka amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyomtaka kutotenda kosa kwa mwaka mmoja, na kutotoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama
Hii ni mara ya pili kwa Shekhe Ponda kuwasilisha ombi hilo baada ya ombi la awali kutupiliwa mbali kwa kuwa kiapo kilichounga mkono ombi kilikuwa na kasoro za kisheria ambazo haziwezi kurekebishika.

No comments: