Wednesday, March 12, 2014

CHANGAMOTO KATIKA KUPAMBANA NA UJANGILI DHIDI YA TEMBO ZATAJWA...

Rais Jakaya Kikwete amesema changamoto mojawapo iliyopo nchini katika kupambana na ujangili, ni ukubwa wa hifadhi na kutokuwa na rasilimali watu wa kutosha.

Rais Kikwete alisema hayo jana wakati akipokea msaada wa magari mapya 11 aina ya Land Rover kutoka kwa Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) la nchini Ujerumani.
Alisema kati ya eneo lote la nchi lenye ukubwa wa kilometa za mraba takribani 945,000, eneo la kilometa za mraba 159,817.02 ni maeneo ya hifadhi ambayo yana wanyama kama
tembo ambao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ujangili.
Alisema licha ya kuwa na eneo kubwa la hifadhi, lakini rasilimali watu ni wachache ambapo kwa wastani, mtu mmoja anasimamia kilometa za mraba 168 wakati kwa viwango vya kimataifa mtu mmoja kusimamia kilometa za mraba 25 pekee.
Rais alisema rasilimali watu waliopo ni asilimia 24 pekee ya wanaohitajika ambao ni 4,000, hivyo juhudi zimeanza kwa kuajiri watumishi hao na lengo linatarajiwa kufikiwa mwaka 2016.
"Baada ya kuajiri rasilimaliwatu wa kutosha, changamoto itakayobakia ni vifaa na mafunzo maalum katika kukabiliana na vitendo hivi vya ujangili ninazidi kuwasihi marafiki zetu hawa kuendelea kutusaidia ili kufikia malengo yetu ya kushinda vita hivi na siyo kushindwa," alisema Rais Kikwete.
Alisema sekta ya utalii inachangia katika Pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 17 huku ikitoa ajira kwa wananchi zaidi ya 300,000 na kusisitiza operesheni mbalimbali za kupambana na ujangili zitaendelea.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema Operesheni Tokomeza inatarajiwa kuanza wakati wowote na siyo siri mara itakapoanza itatangazwa.
Aliwataka wafugaji katika maeneo hifadhi kutoa mifugo yao kwani hawaruhusiwi kisheria na watakaokutwa ndani ya hifadhi katika operesheni hiyo, wawe mifugo au watu hawataachwa.
Nyalandu alisema msaada huo wa magari ni sehemu ya mchango wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotolewa na taasisi za kijerumaini ambazo jumla yake ni Euro milioni 20 kusaidia kukabiliana na ujangili nchini.
Mkurugenzi  FZS Afrika, Robert Muir alisema magari matano kwa ajili ya hifadhi ya Serengeti, matano kwa asili ya Kanda tano katika hifadhi za Selous na moja kwa ajili ya hifadhi ya Maswa.
Alisema msaada inalenga kuongeza nguvu katika kupambana na majangili hao baada ya kushiriki katika sensa iliyofanyika hivi karibuni na kubaini kupungua kwa kasi kwa idadi ya tembo nchini.

No comments: