Sunday, March 23, 2014

ASKOFU KILAINI ATAKA WANAOTAFUNA SADAKA WAFUNGWE GEREZANI...

Askofu Method Kilaini.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini amesema baadhi ya waumini na viongozi wa makanisa wanaoiba fedha za miradi, sadaka na mali nyingine za kanisa, wachukuliwe hatua za kisheria kama wezi wengine.

Kauli hiyo ya Kilaini ameitoa huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa waumini wa madhehebu ya Kikristo nchini ya kuwepo kwa baadhi ya viongozi na wasimamizi wa miradi kuchakachua fedha zinazochangwa ama na waumini au wafadhili kwa maendeleo ya kanisa.
"Ikiwa watu wa aina hii wamo katika makanisa, wanapaswa waonywe, wakishindikana washitakiwe kama wezi wengine maana wanatia aibu kanisa la Mungu, fedha za kanisa iwe ni za miradi au sadaka, zinapaswa kutumika kwa uwazi na kwa faida ya waamini si mtu binafsi," alisema Kilaini.
Akizungumza na mwandishi jana kwa simu, Askofu Kilaini huku akitoa mfano wakati akiwa Askofu Msaidizi Jimbo Kuu la Dar es Salaam, alisema wao waliamua kuweka mwongozo wa fedha unaotaka uwajibikaji na ripoti ilipaswa kufikishwa jimboni.
Kwa uzoefu wa Dar es Salaam, Kilaini alisema unawezesha uwazi katika miradi na fedha za kanisa na kuongeza kuwa, kazi ya usimamizi hufanywa na Paroko, Msaidizi wake wakishirikiana na Kamati Tendaji ya Parokia wakiwemo wenyeviti na waweka fedha wa kanisa na kila senti moja inayotumika inapaswa kuelezwa katika ripoti mara kwa mara.
Askofu huyo alisema ikiwa watu wa kanisa hawaelezi bayana taarifa za mapato na matumizi kwa waumini bila kusubiri kuulizwa, kuna uwezekano wa kuchakachua, fedha za kanisa hazitakiwi ziwe za siri, kama kuna siri lazima kuna wizi. "Kama hatuwajibiki kwa uaminifu vya duniani, tusitarajie kupewa vya mbinguni".
Alisema kuna watu kwa kukosa kujipanga vizuri enzi za utumishi wao wa umma, wanastaafu wakiwa hawana kitu hivyo wanatumia makanisa kama sehemu ya kula pensheni zao kwa kuiba huku akisema wengine ni vijana wadogo wanaotakiwa kusaidia ustawi wa nyumba ya Mungu, lakini wanaiba kanisani.
"Tutawezaje kuwakosoa wengine kama sisi wa kanisani tunaiba? Watu waache kudokoa fedha za kanisani ni laana, watu wa aina hii wanapaswa kuchukuliwa hatua kama mwizi yeyote, wasionewe huruma, kama inavyopaswa kusimamia fedha za umma kwa uaminifu na fedha za kanisa zisimamiwe vivyo hivyo," alisisitiza Kilaini.
Kwa muda mrefu sasa, waumini wa makanisa mbalimbali nchini wamekuwa wakilalamika kuwepo kwa baadhi ya viongozi wao kutumia vibaya fedha za kanisa kwa faida zao binafsi na kwa makanisa mengine hali hiyo imeibua vurugu na kusababisha uvunjifu wa amani.
Pamoja na uwepo wa malalamiko hayo katika baadhi ya Parokia za Kanisa Katoliki, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kanisa la Anglikana, katika Kanisa la Moravian, Jimbo la Misheni Mashariki, kumekuwa na mgogoro kwa zaidi ya miaka miwili sasa, ukihusisha mali na madaraka, jambo lililofanya uongozi wa dunia wa kanisa hilo (Unity Board) kuingilia kati.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa Kanisa la Moravian, jimbo hilo, Mchungaji Emmaus Mwamakula hivi karibuni alinukuliwa akisema kuwa, uroho wa mali na matumizi mabaya ya fedha za kanisa na madaraka, ni moja ya sababu zinazoleta migogoro katika makanisa likiwemo kanisa lao.
Mchungaji Mwamakula alisisitiza kuwa, maombi ya kweli yanahitajika ili baadhi ya viongozi wa kanisa wasio na hofu ya Mungu watambue umuhimu wa uwazi katika uwajibikaji hasa matumizi ya fedha.
Alisema ni haki ya waumini kupata taarifa za mapato na matumizi ya fedha wanazotoa kanisani kila wakati na kufanya tathimini ya kila fedha ili kuongeza imani katika utendaji wa kazi na uwajibikaji wa wasimamizi.

No comments: