NYARAKA ZA MAHAMAKA ZAHIFADHIWA KWENYE CHOO MPANDA...

Mahakama  ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi  imefunga choo chake kwa matumizi yaliyokusudiwa, badala yake  choo kinahifadhi nyaraka mbalimbali za mahakama hiyo.

Aidha, wilayani Ukerewe  katika Mkoa wa Mwanza, Mahakama ya Mwanzo Bukonyo, inakabiliwa na uchakavu wa majengo.
Hali hiyo inadaiwa nyoka huvuruga shughuli za mahakama, kutokana na kudondoka kutoka kwenye paa chakavu, ambako wamejitengenezea makazi.
Matukio hayo yanayoikumba idara ya mahakama, yalibainishwa jana na wadau kwenye maeneo tofauti nchini kwenye maadhimisho  ya Siku ya Sheria  nchini.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo  Bukonyo wilayani Ukerewe,   Malisel  Ndimila, alisema   tangu  apelekwe  katika mahakama  hiyo mwaka jana  hadi sasa,   amenusurika  kuumwa na nyoka  katika matukio  matano tofauti.
Alisema  katika matukio  hayo,  nyoka hao  hutokea juu  ya  dari ya  jengo  la mahakama  hiyo  na  huanguka  chini wakati  mwingine  shughuli za mahakama  zikiendelea  na kusababisha  mtafaruku mkubwa. 
Hakimu Mkazi  Mfawidhi  wa  Mahakama ya Wilaya,   Faustin  Kishenyi  alithibitisha matatizo hayo ya mahakama. Alisema  mbali ya  hali mbaya ya uchakavu  wa majengo ya mahakama,  pia  watumishi wote  wakiwemo  mahakimu  wote wanne na yeye hawana  nyumba.
Mkuu wa Wilaya  ya Ukerewe, Mery  Tesha  alikiri  kuwa  matatizo hayo  yanatokana na ufinyu wa  bajeti. Alitaka wadau kushiriki kutatua matatizo hayo. Alisema serikali  inatambua  umuhimu  wa idara hiyo.
Kwa upande wake Mahakama ya Wilaya  ya Mpanda mkoani Katavi, Hakimu Mkazi  Mfawidhi  wa mahakama hiyo, Chiganga Ntengwa  alisema kutokana na uchakavu wa majengo  na uchache wa ofisi, huwalazimu watumishi  kufanyia shughuli zake kwenye vyumba vya stoo huku choo kikitumika kuhifadhi nyaraka.
Alisema mahakama zote zilizoko wilayani Mpanda,  majengo yake  yaliyokuwa yakitumika  tangu enzi za mkoloni, yamechakaa  na kusababisha  baadhi ya   Mahakama za Mwanzo kufungwa. Alitaja  mahakama  za mwanzo zilizofungwa kutokana na uchakavu ni  Kabungu, Shanwe na Mwese.
Kaimu  Katibu  Tawala wa Mkoa wa Katavi, Lauteri Kanoni  aliyemwakilisha  Mkuu wa Mkoa kwenye maadhimisho hayo,  alisema  Serikali  imeanza  kushughulikia  changamoto  kadhaa  zinazokabili mahakama  hiyo.

No comments: