NECTA YAFAFANUA ALAMA ZA UFAULU MATOKEO YA KIDATO CHA NNE...

Dk Charles Msonde.
Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) limetoa ufafanuzi kuhusu viwango vya ufaulu, alama ya chini ya ufaulu na ufaulu wa jumla, ambavyo vimetumika kwa mara ya kwanza mwaka huu.

Akifafanua kuhusu viwango vya ufaulu jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk Charles Msonde alisema kuanzia mtihani wa kidato cha nne ya mwaka 2013, Baraza limetumia utaratibu wa makundi saba, tofauti na miaka ya nyuma, ambapo walikuwa wakitumia makundi matano.
Alitaja makundi hayo na alama zake kwenye mabano kuwa ni A (75-100) yenye pointi 1; B+ (60-74) yenye pointi 2; B (50-59) yenye pointi 3; C(40-49) yenye pointi 4; D (30-39) yenye pointi 5; E (20-29) pointi 6 na kundi F (0-19) yenye pointi 7.
"Utaratibu huu umelenga kupunguza mlundikano mkubwa wa alama katika kundi mmoja."
"Idadi ya makundi ya ufaulu hutofautina kati ya nchi na nchi kulingana na mahitaji, mfano Kenya wanamakundi 12, Uganda, Malawi na nchi za Afrika Magharibi wanamakundi tisa," alisema.
Alisema kutokana na makundi hayo, kiwango cha mwisho cha ufaulu ni gredi D na kiwango cha juu ni A kwa somo husika na watahiniwa waliopata gredi E na F wanakuwa hawajafaulu somo husika.
Akizungumzia upangaji wa madaraja ya ufaulu, Msonde alisema yamepangwa kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani Kifungu cha 20 (1-6), ambacho kinaeleza kuwa ufaulu katika daraja la Kwanza hadi Tatu unapangwa kwa kuzingatia jumla ya pointi.
Alisema kwa upande wa daraja la Nne, kanuni inataka kupangwa kwa kuzingatia ufaulu wa chini ambao ni gredi D katika masomo yasiyopungua mawili au ufaulu kwa kiwango cha chini ya gradi C katika somo moja.
Hata hivyo, kanuni inaelekeza kuwa ufaulu wa grade A hadi C utakuwa ni ufaulu wa 'Credit' na gredi D inaesabika kuwa ni 'pass' na gredi E na F ni alama za kufeli.
"Tumepokea maswali mengi sana hasa kwa katika daraja la Nne maana wengine wanaonekana kuwa na pointi za daraja sifuri lakini wanaonekana kuwa katika daraja la Nne, kwa kanuni daraja la Nne hupangwa kwa alama za chini na si kwa pointi," alisema.
Msonde alitolea mfano mtahiniwa ambaye amefanya masomo saba na amepata alama D katika masomo mawili na masomo matano amepata F, kwa pointi mtahiniwa huyo ataonekana kuwa na pointi 45 ambazo ni za daraja Sifuri, lakini kutokana na kuwa na D mbili kanuni inamtaka kupewa daraja la Nnne.
Aidha, Msonde alisema kuwa ufafanuzi wa sifa za kujiunga na mafunzo katika ngazi mbalimbali kwa kutumia mfumo huu utatolwa na Kamishna wa Elimu.

No comments: