MWILI WA MTU WAKUTWA UMENASA KWENYE MAGURUDUMU YA NDEGE...

Mwili wa mtu umegundulika kwenye sehemu ya magurudumu ya ndege ya South African Airways iliyokuwa imeegeshwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Washington Dulles huko Virginia.

Mamlaka ya viwanja vya ndege vya Washington ilisema mwili huo wa mwanaume wa makamo uligunduliwa Jumamosi majira ya saa 7:30 usiku na  wafanyakazi wa uwanjani hapo waliopangiwa kushughulikia ndege hiyo.
Ndege hiyo aina ya Airbus A340 ilikuwa imeegeshwa kando ya eneo la maegesho wakati huo.
Kwa mujibu wa maofisa wa uwanja huo wa ndege, mazingira ya kifo cha mtu huyo yanafanyiwa uchunguzi kwa sasa. Mwili huo utapelekwa kwa uchunguzi katika ofisi ya Fairfax County Medical.
Maofisa walisema shughuli katika uwanja huo wa ndege haukuathiriwa na kugundulika huko kwa mwili huo.
Polisi wa uwanjani hapo na vikosi vya zimamoto walifika eneo la tukio sambamba na wapelelezi wa FBI na maofisa wa Forodha na Ulinzi wa Mipaka.
Tlali Tlali, msemaji wa South African Airways, alieleza kwamba ndege yanye usajili wa SA 207 ilitokea Johannesburg na kutua uwanja huo wa Dulles Jumatano baada ya kuwa imetua mjini Dakar, Senegal.
"Tunasikitika kwa kupotea kwa maisha ya binadamu yeyote na tunashughulikia kwa kina fununu zzote zinazohusiana na tukio hilo...," alisema Tlali kwenye taarifa.
Dulles, iliyoko maili 25 magharibi mwa Capitol, ni moja ya vitovu vya safari vyenye pilika nyingi nchini humo kikipokea zaidi ya abiria milioni 22 kwa mwaka.

No comments: