MAMIA WAAGA MIILI YA ASKARI WATANO WALIOKUFA AJALINI DODOMA...

Miili ya askari hao ikiombewa katika ibada maalumu kabla ya kusafirishwa makwao kwa mazishi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime jana aliongoza mamia ya waombolezaji kuaga askari polisi watano waliokufa ajalini  na kusema vifo vya askari hao vimetokana na uzembe na mwendo kasi.
Alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kuwasili kwa miili ya marehemu hao kabla ya kusafirishwa kila mmoja kwenda kwao.
Marehemu hao ni D.9084 Adolf Silla (51) aliyesafirishwa kwenda Kongwa, F.6459 Evarist Bukombe (34) kwenda Kigoma, H.3783 Deogratius Mahinyila (29) kwenda Mpwapwa,  WP.10337 Jackline Tesha (22) kwenda Kilimanjaro na WP.10382 Jema Luvinga aliyesafirishwa kwenda Iringa. 
Kwa mujibu  wa Misime, miili hiyo iliharibika, hali iliyolazimu madaktari wa hospitali ya Rufaa ya Dodoma kufanya kazi ya ziada kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ili iweze kusafirishwa hadi walikozaliwa askari hao.
Alitaka kila mtu kuwa balozi, kuhakikisha ajali za barabarani ambazo asilimia 75 zinasababishwa na uzembe zinakoma, la sivyo wataendelea kusingizia kuwa vifo hivyo vinasababishwa na Mwenyezi Mungu.
Alisema  wakati mwingine watu wanaharakisha kifo hasa pale unapokuwa si mpango wa Mungu kuondoka duniani kutokana na uzembe.
"Hata ukiona gari lile lilivyoburuzwa unaamini kabisa kilichosababisha ni mwendo kasi," alisema Misime. Alisema msiba huo ni mkubwa, kwani umepoteza nguvu kazi, walinzi na hivyo jamii kukosa watu wa kuwahudumia kutokana na  uwiano wa askari mmoja kuhudumia idadi kubwa ya watu.
Askari hao walikufa papo hapo usiku wa kuamkia juzi baada ya gari waliyokuwa wakisafiria, T.770 ABT Toyota Corolla  kugongana uso kwa uso na basi T.997 AVW Scania mali ya Kampuni ya Mohamed Trans.
Ajali ilitokea katika Kijiji cha Mtumba, Manispaa ya Dodoma wakati askari hao wakitoka Dodoma kwenye sherehe za Polisi za kuaga mwaka 2013 na kukaribisha 2014.

No comments: