Januari Makamba (kushoto) na Stephen Wassira. |
Jana ilikuwa zamu ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Steven Wassira.
Hiyo ni baada ya juzi Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja kuhojiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza mahojiano yaliyofanyika katika jengo la makao makuu ya CCM maarufu kama White House mjini hapa, Januari ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema hakukuwa na mashitaka bali ushauri.
Alisema ushauri huo ulihusu namna ya kupata viongozi kwa ajili ya kuimarisha chama badala ya kukigawa hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.“Hakukuwa na habari ya mashitaka bali kutoa ushauri na kukumbushana misingi ya namna ya kupata uongozi na kuimarisha chama badala ya kukigawa,” alisema.
Januari alisema binafsi amefurahi kupata nafasi ya kuitwa na kutoa ushauri.Alisema hiyo ilikuwa ni fursa nzuri kwake kutoa mawazo na maoni yake, lakini hata hivyo alishangaa kuitwa Dodoma kujieleza.
Pia alisema kuna faida kubwa ya kujulikana mapema kuliko mwishoni, kwani watu wanapata nafasi ya kukujadili na kutoa mawazo yao kama unafaa kuwa kiongozi au la.
“Mbaya kama unatoa fedha inakuwa unawaweka pembeni watu wenye vipaji vya uongozi,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa sheria za nchi, mtu anapotumia fedha kupata uongozi ni lazima sheria ichukue mkondo wake na achukuliwe hatua.
“Kuitwa ni jambo la kawaida, hakuwezi kutoa sababu ya wewe kujitafakari na kujipima,” alisema.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu, Steven Wassira akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka katika mahojiano hayo, alisema hajawahi kutangaza nia ya kugombea urais na wala si dhambi mtu kutamani kuwa Rais wa Nchi.
Wassira alisema hakuitiwa tuhuma ila waandishi wa habari wamefanya mkutano uwe wa tuhuma lakini amesema wamezungumzia juu ya mustakabali wa kuelekea uchaguzi mkuu 2015.
Alisema magazeti mengi yaliripoti kuwa wanaitwa kwa tuhuma ya kutangaza nia kabla ya wakati.
"Sijawahi kutangaza kugombea Urais, kwani ni kosa kutangaza kugombea Urais?" alihoji Wassira na kuongeza:
"Kuna barua na magazeti ambayo yanatofautiana juu ya kuitwa Dodoma, andikeni ukweli mimi ni mjumbe wa Kamati Kuu siwezi kuvuruga chama.”
Alipohojiwa kwa nini wameitwa wanachama sita tu, alisema hafahamu idadi ya wanachama walioitwa kuhojiwa isipokuwa anachojua yeye kama Wassira
ameandikiwa barua na kuitwa Dodoma.
"Sio dhambi kutamani kuwa Rais, kwani ni nafasi moja kwa Watanzania wote na kila mtu anayo haki ya kuomba nafasi hiyo ila utaratibu ufuatwe," alisema.
Hata hivyo alisisitiza kuwa hajawahi kutangaza nia.
Huku akiwa na mbwembwe za aina yake hasa pale waandishi walipoanza kumpiga picha alisema: "Mimi sijatangaza nia na sina muda wa kutangaza leo mpaka wakati ukifika, huku akisogea kupigwa picha na kutaka apigwe picha nyingi.
"Pigeni picha nyingi , pigeni mpaka mchoke mkimaliza ndio niondoke," alisema.
Kamati hiyo inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara, Philip Mangula, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Hatua ya kuhojiwa kwa wanachama hao, inatokana na agizo la Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete likitaka kamati za usalama na maadili za chama hicho kubana wanachama wanaokiuka maadili.
Baada ya kuhojiwa juzi, Lowassa aliwaambia waandishi wa habari: "Tumeshauriana na kukubaliana vizuri tu, ili kukisaidia chama kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015," na kuongeza: "Sijibu lawama, kwa vile hakikuwa kikao cha lawama, kilikuwa cha mazungumzo na ndani ya kikao hakukuzungumzwa makundi."
Sumaye kwa upande wake, aliwaambia waandishi kuwa hawezi kusema lolote kuhusu kilichojiri ndani ya kikao hicho na badala yake anasubiri wakubwa (Kamati) wazungumze ndipo naye aseme.
Mbunge Ngeleja alisema chama kina utaratibu wake na taarifa ya kikao hicho itatolewa na msemaji wa chama.
"CCM ni chama chenye Katiba na kanuni zake na wakati wa kutangaza nia ndani ya CCM bado haujafika," alisema.
Alisema kwa mujibu wa CCM, wao wanaongozwa na kanuni, na wenye nia ya kugombea muda haujafika na si jambo la ajabu chama kuita watu wake kuwahoji.
"Binafsi sijatangaza nia ya kugombea urais… kama kuna ugomvi mimi siko kwenye ugomvi huo," alisema Ngeleja.
Wengine wanaosubiri kuhojiwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
No comments:
Post a Comment