CCM NA CHADEMA ZAKABANA KOO UCHAGUZI MDOGO KATA...

Masanduku ya kura.
Uchaguzi mdogo katika kata 27 umefanyika nchini jana, ambapo mchuano mkubwa katika uchaguzi huo karibu katika kata zote, ulikuwa kati ya CCM walioonekana kupata ushindi katika kata nyingi na kufuatiwa na Chadema iliyokuwa ikitoa ushindani mkali.

Mkoani Kilimanjaro katika uchaguzi wa Kata ya Kiboriloni, Chadema ilishinda baada ya kumbwaga mgombea wa CCM kwa kura nyingi.
Msimamizi wa Uchaguzi katika kata hiyo, Shaban Ntarambe, alimtangaza mgombea wa Chadema, Frank Kagoma, kuwa Diwani wa Kiboriloni baada ya kuibuka kidedea kwa kupata kura 1,019. Taarifa zaidi zilieleza kuwa Chadema pia imepata pia ushindi katika Kata ya Njombe Mjini, mkoani Njombe.
Kagoma alimshinda Willy Aidan wa CCM, aliyeambulia kura 255 na Aidan Mzava wa UDP aliyeambulia kura 2.
Katika Kata ya Sombetini mkoani Arusha, mpaka tunakwenda mitamboni, mgombea wa Chadema Ally Bananga, alikuwa akiongoza dhidi ya mgombea wa CCM, David Molel na mgombea wa CUF, Ally Mkali.
Mkoani Shinyanga, Kata ya Ubagwe alishinda mgombea wa CCM, Hamis Mbogola, ambaye alipata kura 328 dhidi ya mgombea wa Chadema, Adam Ngombale, aliyeambulia kura 219.
Mkoani Morogoro katika Kata ya Tungi, Mgombea wa CCM, Mzeru Paulo, alishinda baada ya kupata kura 715 na kuwashinda wengine akiwemo wa Chadema, Juma Tembo aliyepata kura 416.
Hata hivyo katika uchaguzi huo, wapigakura wachache walijitokeza kupiga kura kwakuwa kati ya wapigakura  4,667 waliojiandikisha kupiga kura, ni wapigakura 1,205 waliojitokeza kupiga kura.
Taarifa tulizopata wakati tunakwenda mitamboni, zilieleza kuwa CCM imeshinda katika Kata ya Magomeni Bagamoyo, Kata ya Kiomoni, Tanga; Kata ya Mtae Lushoto na Kata Nduli, Iringa.
Vurugu za hapa na pale zilitokea hasa katika uchaguzi wa udiwani Kata ya Sombetini mara baada ya Mbunge wa Arusha  Mjini, Godbless Lema (Chadema) kufika Ofisi  Kata  ya Sombetini na kutaka  Katibu wa  CCM, Kata ya Sombetini, Gerald Munisi akamatwe na Polisi.
Munisi alikuwa akidaiwa kumsaidia baba mmoja ambaye alionekana kuwa na matatizo ya miguu aliyekuwa na gari lenye namba za usajili T751 ALY aina ya Starlet.
Munisi alimsaidia mtu huyo aliyedai kuwa ndugu yake
kwa kumshusha na kumpeleka hadi kwenye kituo cha kupigia kura na alimsubiri apige kura akiwa nje ya kituo na alipokuwa akitoka ndipo alipokutana na purukushani hiyo kati ya Lema na wafuasi wa Chadema pamoja na wafuasi wa CCM.
Munisi alisema amefika hapo kumsaidia baba huyo ili apige kura lakini Lema alilalamika kitendo cha Polisi kumuona Munisi zaidi ya mara nne akileta watu tofauti mara kadhaa kudai kuwasaidia.
"Kwani kuna nini nikimsaidia mtu tena ni ndugu yangu nanyi si mnamuona? Kwanini tuhisiane vibaya niacheni niondoke," alisikika akisema kiongozi huyo wa CCM.
Lema naye alimuasa Munisi kuondoka eneo hilo kwani watu si wajinga na wameona tabia hiyo mara kadhaa hivyo si busara kwa kiongozi wa CCM kufanya hivyo.
Baada ya kurushiana maneno ya hapa na pale Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha, Gilles Muroto alimsihi Lema na Munisi kuondoka eneo hilo kwani wanasababisha vurugu na kuleta hofu kwa wapigakura.
Vijana kadhaa walionekana maeneo mbalimbali ya vituo vya kupigia kura meta 100 kutoka kituoni wakiangalia jinsi uchaguzi unavyofanyika huku polisi nao wakiimarisha ulinzi katika vituo mbalimbali jijini hapa.

No comments: