VIONGOZI WA DINI WAINGIA MAKUBALIANO NA SERIKALI KWENYE GESI...

Rais Jakaya Kikwete katika picha ya pamoja na viongozi wa dini walioshiriki katika kongamano hilo.
Serikali imeanzisha utaratibu wa kusimamia rasilimali za nchi kwa kushirikiana na viongozi wa dini, ili kuondoa upotoshaji na kuimarisha umoja na amani ya nchi.
Rais Kikwete alisema hayo jana katika kongamano lililoandaliwa Dar es Salaam na viongozi wa dini nchini, kuhusu rasilimali za gesi asilia, mafuta na madini.
 “Serikali ikiongozwa kwa ubia wa namna hii, tutafika mbali…nimezungumza na viongozi mambo mengi tuyasimamie kwa utaratibu huu,” alisema Rais Kikwete.
Awali akizungumza katika kongamano hilo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga, alisema viongozi wa dini waliamua kuandaa kongamano hilo baada ya kubaini upotoshaji juu ya suala la uchimbaji wa nishati hizo.
Alisema pamoja na kwamba lengo hasa ni kuangalia eneo la mazingira, lakini pia viongozi hao walitaka kuwepo na utaratibu wa mazungumzo, ambao utabainisha mipango ya Serikali katika maslahi ya rasilimali hizo na eneo la utunzaji mazingira.
“Tunafahamu kuwa gesi na mafuta ni vichocheo vikubwa vya maendeleo, lakini nchini vimeleta hisia hasi kwa jamii, tumekuwa tukisikia taarifa potofu kuhusu suala hili, hali iliyoleta usumbufu mkubwa; kama viongozi wa dini tunaomba watu wasitumie fursa hii kujipatia umaarufu na kupotosha,” alisema.
Alisema wanashukuru walipofika kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliwaeleza ukweli wa manufaa na changamoto zilizomo kwenye sekta ya gesi.
“Ametueleza nia ya kusambaza gesi Dar es Salaam na nchi nzima na kubadili biashara ya magunia 40,000 ya mkaa yanayotumika kwa siku katika Jiji la Dar es Salaam,” alisema Askofu Munga.
Alisema kwa kufuata utaratibu huo, matakwa ya watu binafsi hayawezi kupewa kipaumbele kwa kuwa  viongozi wa dini, wanataka rasilimali zisaidie wananchi.
Mjumbe wa Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Shekhe Hamid Jongo, akizungumzia utaratibu huo, alisema viongozi hao wana jukumu la kufikisha kwa Watanzania ukweli walioupata.
“Nimegundua faida nyingine, kuwa badala ya viongozi wa dini kukaa vikao vya kutengenezeana mishale na kuelekezeana, tunaweza kukaa pamoja tukapika mseto na kula pamoja,” alisema.
Profesa Muhongo, alisema utafutaji wa gesi na mafuta nchini ulianza mwaka 1952 ambapo Mwalimu Julius Nyerere aliweka misingi mizuri ya kusimamia rasilimali hiyo kwa lengo la kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika.
Alisema katika misingi hiyo, Mwalimu Nyerere aliweka njia nzuri na namna sahihi ya kugawana rasilimali hizo.
“Sasa sidhani ile saini ya Nyerere ilionesha mwekezaji wa nje afaidike kuliko wa ndani, naomba mtusaidie tusije tukapotoshwa na kupigania maslahi ya mtu na familia yake,” alisema.
Akifafanua kuhusu hilo, Rais Kikwete alisema pamoja na kwamba Tanzania imejaaliwa utajiri mkubwa wa rasilimali za asili kama vile madini, misitu, wanyamapori, gesi na ardhi kubwa kuliko nchi zote za Afrika, bado kuna changamoto ya kuhakikisha rasilimali hizo hazigeuki laana na chanzo cha vurugu.
Alisema tayari migogoro ya ardhi imeanza kujitokeza baina ya wakulima na wafugaji na wahifadhi wa misitu, mbuga za wanyama na vitendo vya kuuawa hasa kwa tembo kiholela hali ambayo pamoja na kusababisha vurugu pia imesababisha vifo.
“Ni wakati mwafaka wa kutafakari ni jinsi gani rasilimali hizi zitalindwa na kutumia vizuri, tusipokuwa makini rasilimali hizi zinaweza kugeuka chanzo cha mfarakano na laana kwa nchi badala ya neema, sipendi kuona rasilimali hizi zinageuka na kuwa laana ya Tanzania,” alisema.
Alisema tangu Tanzania ipate uhuru Serikali imekuwa ikisimamia rasilimali asili kwa umakini ili kuhakikisha Watanzania wote wananufaika nazo kwa kuunda sheria na sera za kusimamia utajiri huo.
Rais Kikwete alisema moja ya mikakati ya kuhakikisha gesi hiyo inanufaisha Watanzania, ni kutumia sehemu kubwa ya nishati hiyo nchini na kupelekwa katika viwanda vikubwa vya mbolea na saruji Mtwara na nyingine kusambazwa majumbani na viwanda vingine nchini.
“Tunafahamu kuwa tunakabiliwa na tatizo la mazingira kutokana na matumizi makubwa ya miti, gesi hii tukiitumia vizuri italitoa Taifa kwenye umasikini, tunataka Tanzania iondokane na matumizi ya kuni na mkaa,” alisema.
Rais Kikwete alionesha kusikitishwa na namna baadhi ya wanasiasa walivyopotosha suala la matumizi ya gesi ambapo pamoja na kufahamu mikakati ya Serikali kwa makusudi ya kujipatia umaarufu wa kisiasa walipotosha Watanzania.
“Nimeomba waniambie ni nchi ipi ambayo imepasuliwa vipande vipande kutokana na rasilimali,” alisema Rais Kikwete na kumshukuru Mungu kwa kuwa yeye hajawa mwanasiasa wa aina hiyo.
Aidha, alisema katika kuhakikisha gesi hiyo inatumika na kunufaisha vizazi vijavyo, Serikali ina mpango wa kuanzisha mfuko maalumu wa mapato ya gesi ambao utaweka viwango maalumu vya mapato hayo kutumika kwenye bajeti ya nchi na fedha nyingine kutunzwa kwa ajili vizazi vijavyo.

No comments: