TATIZO LA UPATIKANAJI MAJI DAR KUBAKI HISTORIA KUANZIA MACHI...

Wachuuzi wa maji katika moja ya maeneo ya Dar es Salaam wakiwa kazini.
Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanatarajiwa kuondokana na tatizo la upatikanaji wa maji safi kwa asilimia 90 kuanzia Machi baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bomba la Ruvu Chini na mtambo wa maji ulioko Bagamoyo.

Akizungumza juzi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO), Jackson Midala alisema ujenzi wa bomba hilo utakamilika mwezi ujao na mtambo umekamilika kwa asilimia 99.
"Mtambo huo wa Ruvu Chini mwanzoni ulikuwa ukipitisha lita za maji 180,000 kwa siku lakini utakapokamilika utapitisha lita 270,000 kwa siku hivyo kwa asilimia 90 tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam litakuwa limetatuliwa," alisema Injinia Midale.
Alisema kazi ya kulaza bomba jipya Ruvu Chini imekamilika kwa asilimia 60 mpaka sasa na hivyo maeneo yaliyokuwa na tatizo la maji kama Ubungo, Tandale, Goba na maeneo mengine tatizo la maji litakuwa historia.
"Mtambo huo umeshaanza kufanyiwa majaribio, lakini pia tunajenga bwawa la Kidunda, Morogoro ambalo litasaidia kuhifadhi maji ya Mto Ruvu ambayo yanapotea kwa kiasi kikubwa kwa kuingia baharini," alisema.
Aidha alisema wakati huo huo bwawa hilo litasaidia pia kutoa umeme megawati 20 ambazo zitasaidia kuendeshea mtambo na pia kwa matumizi ya wakazi wa Morogoro.
Alisema katika eneo la Kimbiji Shirika hilo linachimba visima vya maji kwasababu ni eneo ambalo limeonekana kuwa na maji mengi kwa ajili ya kusaidia watu wa eneo la Kigamboni.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika Mei mwaka jana bungeni alisema upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam umekuwa ni tatizo kiasi kwamba katika maeneo fulani wakati maeneo mengine upatikanaji wake ni kwa mgawo huku wengine kupata usiku wa manane tu wakati maeneo mengine hawajui shida ya maji na kuhoji mikakati ya serikali kutatua tatizo hilo.
Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge alijibu Serikali imekuja na miradi ya kuboresha Ruvu Chini na Ruvu Juu pamoja na visima hata hivyo alisema upungufu wa maji unasababishwa pia na upotevu wa maji unaosababishwa na watu wanaoliibia shirika.

No comments: