SASA HALMASHAURI YA JIJI PEKE YAKE KUSIMAMIA MAEGESHO DAR...

Maegesho ya magari kando ya Barabara ya Samora.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imezinyang'anya rasmi Manispaa majukumu ya kusimamia maegesho ya magari na imefuta vibali vyote vya maegesho  vilivyotolewa na mamlaka hizo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Kamati ya Ushauri Mkoa wa Dar es Salaam (RCC) kuagiza halmashauri ya Jiji  kufanya kazi hiyo baada ya kubaini  halmashauri za Ilala, Kinondoni na Temeke, kisheria hazikupaswa kusimamia maegesho ya magari.
Aidha, RCC imeamua kusitisha mikataba ya usimamizi ya manispaa hizo na kuagiza jiji lisimamie maegesho, baada ya kubaini mawakala waliokuwa wamepewa kazi hiyo, walikuwa wakibughudhi  madereva na wamiliki wa  magari  kwa kuwatoza faini bila kuzingatia utaratibu, kuvizia na kukokota magari kwa ubabe.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji, Wilson Kabwe, alisema, "tulishapeleka malalamiko kwamba manispaa zinafanya kazi isiyo yao kisheria. Vile vile waliokuwa wanafanya kazi hii kama mawakala, walikuwa wanatoza faini bila utaratibu."
Alitaja mawakala hao ni Mwamkinga Auction Mart Ltd na Tambaza Auction Mart and General Broker, ambao katika utekelezaji, pia wanashutumiwa kwamba wafanyakazi walitumia lugha chafu kwa wananchi, walivizia magari kuyakamata, kuyafunga na kuyavuta kwa nguvu kupita kiasi na kutoza faini kubwa zisizo na utaratibu.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alipoulizwa ni kwa namna gani manispaa 'zilipora' mamlaka ya jiji na kuanza kusimamia maegesho, alikiri kuwepo kasoro.
"Kama wangechukua (manispaa) ikawa hakuna bughudha kwa wananchi, yawezekana wangeachiwa. Aliyechukua ni mwenzetu, na kwa kuwa tumeona alifanya makosa, umefika wakati wa kumnyang'anya," alisema.
Katika kuanza kutekeleza majukumu, Mkurugenzi huyo wa Jiji alisema wanafanya kazi ya kusimamia maegesho kwa kushirikiana na wakala wake, National Parking Solution (NPS) na kwa kuanzia, vibali vyote vya maegesho ya magari vilivyotolewa na mamlaka zingine vimefutwa. Walio na vibali warudishe halmashauri ya jiji ili wapewe vingine kwa mujibu wa sheria.
Vibali vingine vilivyofutwa ni vya teksi, vilivyotolewa na mamlaka zingine vimefutwa na vitatolewa upya na halmashauri kwa kuwa baadhi ya vituo vipo katika maeneo yasiyostahili. Pia vituo vyote vya teksi visivyo katika mpango wa jiji, vitaondolewa kuwezesha magari kupita kwa urahisi kupunguza msongamano.
Uamuzi mwingine uliotangazwa na jiji ni kwamba maeneo yote yaliyokuwa maegesho ya magari, ambayo yamegeuzwa kwa matumizi mengine, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa majengo mbalimbali katika maeneo ya katikati ya jiji na Kariakoo, yatarajeshwa.
Vile vile magari makubwa ya mizigo kuanzia tani 3.5, yanatakiwa kufuata sheria zilizoainishwa kuhusu kuingia kati kati ya jiji. Pia ni marufuku kwa maguta na mikokoteni yenye mizigo mikubwa kuingia katikati ya jiji. Bodaboda zote haziruhusiwi kuingia katikati ya jiji, ingawa Mkurugenzi Kabwe alisema hilo watashirikiana na polisi.
Wakati inadaiwa mawakala chini ya manispaa walitoza faini hadi takribani Sh 300,000 kwa waliokiuka utaratibu wa maegesho, mkurugenzi wa Jiji ametangaza viwango vipya vya adhabu, watakaokiuka sheria ni kati ya Sh 20,000 na Sh 80,000 kulingana na kosa.
Alitoa mfano wa kwamba faini ya kuvuta gari lililovunja sheria, faini yake haizidi Sh 80,000. Makosa mengine kama vile kutolipa ushuru wa maegesho ya magari na kufunga gari, kuegesha sehemu zisizoruhusiwa, kuingiza gari zaidi ya tani 3.5 katikati ya jiji na kuosha gari kwenye maegesho, faini yake haizidi Sh 50,000.
Makosa mengine ambayo faini yake haizidi Sh 50,000 ni kufanya biashara kwenye maegesho ya magari, kuweka vizuizi kwenye maegesho, kutengeneza magari kwenye magesho na kushusha au kupakia mizigo maeneo ya magesho bila idhini ya halmashauri.  Aidha faini ya kulaza gari lililokamatwa kwa siku ni Sh 20,000.
"Faini lazima ziwepo, lakini kupiga faini au kuvuta gari, zitakuwa jitihada za mwisho. Lazima elimu itolewe kwanza. Wenzetu (mawakala wa manispaa) walitoza kwa kubughudhi watu," alisema.
Akizungumzia ushirikiano wao na NPS, Mwanasheria wa Jiji, Robert Mageni alisema alipatikana kwa ushindani na mkataba wake unaisha Agosti mwakani.  
Kwa mujibu wa makubaliano kati ya NPS na Halmashauri ya Jiji, malipo ya faini zote zitakazotozwa, zitalipwa kwa wakala huyo na baadaye kurejeshwa halmashauri ya jiji kwa utaratibu uliowekwa na sheria za fedha.

No comments: