Stendi Kuu ya mabasi Moshi. |
Hali hiyo inatokana na ulanguzi wa tiketi, unaodaiwa kufanywa na mawakala wa mabasi wa kituo cha mjini Moshi.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya abiria kusitisha safari jana baada ya kushindwa kumudu kiasi hicho cha nauli.
Mwandishi alibaini abiria walikuwa wakitozwa kati ya Sh 40,000 na Sh 50,000 kwa mabasi yanayokwenda Dar es Salaam, tofauti na nauli halali ya kati ya Sh 18,000 na Sh 28,000.
Baadhi ya abiria walimwambia mwandishi kwamba licha ya kutozwa Sh 50,000, kwenye tiketi zao huandikiwa Sh 20,000.
Mmoja wa abiria, Justine Kimario alisema, “Kinachofanyika hapa ni kwamba abiria unapofika, unaambiwa nauli ni Shilingi 40,000 au 50,000 na wakala anakuambia ukiulizwa na Sumatra sema umelipa Shilingi 20,000 ambayo imeandikwa kwenye tiketi, ukikataa tozo hiyo unaambiwa gari imejaa. Na mabasi yote wameshikilia huo msimamo.”
Kimario alisema, “Hatuna jinsi ya kujitetea kwani ukishakata nauli yao ukienda Sumatra wanakukana kutokana na tiketi kuonyesha umelipa Shilingi 20,000 na ukikataa nauli yao hupati gari, sasa inabidi tuumie hivyo ili kuwahi shughuli zetu.”
Mwandishi alifika kituoni hapo jana saa 11 alfajiri na kukuta umati wa abiria, waliotaka kusafiri, lakini kutokana na kutomudu tozo ya nauli, baadhi walisitisha safari.
Mmoja wa abiria aliyesitisha safari yake, Emmaculata Msangi alisema alifika kituoni hapo alfajiri kwa lengo la kupata nauli ya nafuu, kwani juzi hali ilikuwa hivyo na kusababisha kusitisha safari yake. Hata hivyo, jana pia aliahirisha kutokana na kutomudu tozo ya nauli.
Mwandishi pia alishuhudia polisi ambaye jina lake halikufahamika, akilumbana na mawakala wa mabasi katika harakati za kutaka watende haki kwa kutoza nauli elekezi.
“Nyie mawakala mnachofanya siyo ustarabu, mnatesa akinamama na watoto kwa tamaa zenu, sitakubali kuona ulanguzi huu… abiria, mtu yeyote anayelanguliwa afikishe malalamiko Sumatra,” alisema askari huyo akielekeza abiria pa kwenda kuwasilisha malalamiko.
Akizungumza na mwandishi, Ofisa Mfawidhi wa SUMATRA Mkoa wa Kilimanjaro, Fabiani Nyan’goro, alisema jitihada za kukomesha ulanguzi huo zinaendelea.
“Tunajitahidi sana na tunaomba tusaidiane, pia nawaomba abiria kutoa taarifa za haraka katika namba zinazotajwa kwenye vipaza sauti vya stendi, lakini jitihada zinaendelea kuhakikisha biashara hiyo haramu haifanyiki.
No comments:
Post a Comment