KIGOGO ALIYETESWA CHADEMA AKIMBIA NYUMBA YAKE KWA USALAMA...

Josephat Yona.
Mgogoro wa uongozi unaoendelea ndani ya Chadema, umemlazimisha Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kukemea na kutaka pande zinazopingana kuzuia wafuasi kujihusisha na vurugu na uvunjifu wa amani.
Jaji Mutungi alitoa kauli hiyo jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu mgogoro huo, ambao uongozi wa Mwenyekiti Freeman Mbowe, umepiga marufuku viongozi, wanachama na mashabiki wa chama hicho kumwunga mkono aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe.
“Nachukua fursa hii kukemea vurugu na vitendo vya uvunjifu wa amani uliofanywa na wafuasi wa pande zote mbili katika maeneo ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
“Pia kila kiongozi, mwanachama au shabiki wa chama cha siasa aelewe kuwa anawajibika yeye binafsi kwa uvunjifu wowote wa sheria,” alisema Jaji Mutungi.
Mbali na kuwakemea, pia Jaji Mutungi alitoa kauli ya kutilia shaka ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia ndani ya chama hicho.
“Migogoro ndani ya vyama vya siasa ni mojawa ya vyanzo vya uvunjifu wa amani, hivyo nawaasa wadau wote, kwamba migogoro hiyo inapaswa isivuke mipaka na kuwa uhasama na uadui wa kufanya wafuasi wa pande mbili kupigana, kwani hiyo si demokrasia.
“Nasisitiza, kwamba ni vema viongozi na wanachama wa vyama vya siasa waoneshe ukomavu wa kisiasa kwa kushughulikia tofauti zao na migogoro baina yao kwa ustaarabu, utulivu na amani, huku wakizingatia sheria zote za nchi... hiyo ndiyo demokrasia ya kweli,” alisema.
Alisema moja ya majukumu ya ofisi yake ni kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa  ya Mwaka 1992 na kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa za Mwaka 2007, zinazokataza vyama kuruhusu wanachama au mashabiki kujihusisha na vurugu na uvunjifu wa amani.
Aidha, Mutungi aliasa waandishi wa habari kujiepusha kushabikia migogoro ndani ya vyama vya siasa na kutaka watafakari kwa undani athari za taarifa zao kwa jamii, kabla ya kuzitoa hasa kuhusu mgogoro wa ndani ya chama chochote cha siasa.
Wakati wa kusubiri hukumu ambayo uongozi wa Chadema ulishindwa, nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kulikuwa na mvutano  kati ya wana Chadema wanaomwunga mkono Zitto na upande wa akina Mbowe.
Wanachama hao walikuwa wakifurika mahakamani hapo na kujigawa katika makundi mawili na mara kadhaa walipigana na kutoana damu.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Temeke, Josephat Yona, amehama nyumbani alikokuwa akiishi kwa sababu za kiusalama.
Akizungumza jana na mtandao wa millardayo.com, Yona ambaye alishambuliwa Jumatatu na watu wasiojulikana baada ya kutekwa na kupigwa na kutelekezwa, hivi sasa baada ya kutoka hospitalini alikokuwa amelazwa kwa matibabu anaishi kusikojulikana.
“Ni kweli nimehama kwa sababu za kiusalama … wale watu walivyonichukua walinipiga nikawa sijisikii vizuri nilipokuwa naongea na waandishi, lakini leo (jana) niko vizuri, mtu kama (anamtaja jina) alikuwa akiwapigia simu nawasikia kabisa, walikuwa wanawasiliana naye … kuna mtu kama k-two,” alisema Yona.
Aliendelea kulalamika, kwamba kama ameumizwa yeye kiongozi wa chama itakuwaje kwa watu wa chini … “vyombo vya usalama inabidi viangalie hata walionifungia ofisi yangu saa 10 kabla ya mimi kutekwa, kwa sababu ni saa chache tu kabla ya kutekwa”.
Alisema maendeleo yake sasa ni mazuri zaidi ila kichwa na mgongo bado vinamuuma na walikubaliana aondoke hospitali saa 12 jioni siku ya tukio kwa sababu ya mambo ya kiusalama.
Kuhusu madaktari alisema kulingana na vipimo vyao anaendelea vizuri na yamebaki maumivu  kwa sababu ya vidonda na walimpa dawa za kumeza zingine akanunue mtaani.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chama hicho, John Mnyika ametoa taarifa ya kutafuta maoni kuhusu bei mpya ya umeme.
Mnyika ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, alitoa mwito kwa wenye kuathirika na uamuzi huo ndani ya wiki moja kuanzia sasa watume maoni na mapendekezo yao kwa barua pepe kupitia anuani mbungeubungo@gmail.com.
Pia alipendekeza maoni hayo yatumwe kwa njia nyingine za kuwasiliana na Ofisi ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Chadema.

No comments: