Faru akiwa ameuawa mbugani. |
Kasi ya ujangili
imeendelea kuleta hofu dhidi ya rasilimali nchini, baada ya juzi majangili kuua
faru aitwaye ‘Mama Serengeti’ na kumng’oa pembe zake katika Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti.
Aidha, kundi jingine
linalosadikiwa kuwa la majangili, likiwa ndani ya Hifadhi ya Mamlaka ya
Ngorongoro lilivamia basi la abiria na kuwapora wasafiri fedha na mali zao juzi
alasiri.
Kutokana na hali hiyo,
Serikali jana alfajiri ilituma kikosi maalumu cha askari 20 wenye silaha na
vifaa maalumu vya kupambana na ujangili ili kuongeza nguvu na kuhakikisha
majangili hao wanatiwa mbaroni.
Hayo yamethibitishwa na
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu jana alipozungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, huku akisisitiza kuwa, hali ya
ujangili nchini ni mbaya na kwamba, kwa namna yoyote ile Serikali itapambana na
vitendo hivyo vya uhujumu uchumi vinavyofanywa dhidi ya rasilimali za Taifa.
“Tumeagiza kila gari
ama mtu anayeingia na kutoka katika hifadhi ya Serengeti na Ngorongoro
apekuliwe, ikiwa ni sehemu ya kuwasaka wahalifu, tahadhari imetolewa kwa
mwananchi yeyote kutoa taarifa zinazohusu wageni na watu wanaotiliwa shaka,
tuna taarifa ya raia watatu wa nchi moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
hivyo kuonesha dalili kuwa mtandao wa kuua faru ni mkubwa,” alisema Nyalandu.
Akielezea ilivyokuwa,
Nyalandu alisema walipokea taarifa za kusikitisha usiku wa kuamkia jana, saa
6.30 za majangili kuua faru katika eneo la Moru, Kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti na kwamba askari wa wanyamapori waliokuwa doria ndio waliogundua faru
huyo akiwa amepigwa risasi na pembe zake kung’olewa.
Faru huyo ameacha mtoto
mwenye umri wa miezi miwili na mpaka taarifa hiyo ilipotolewa, mtoto huyo
alikuwa hajulikani alipo. Inaelezwa alipewa jina Mama Serengeti kutokana na
kuwa chimbuko na faru wengine 31 `wazalendo’ waliobaki katika Hifadhi ya
Serengeti.
Mbali ya faru hao `wazalendo’,
hifadhi hiyo pia ina faru wengine wanne kati ya watano ambao waliletwa nchini
kwa mradi maalumu uliosimamiwa na Rais Jakaya Kikwete kutoka Afrika Kusini.
Faru mmoja kutoka Afrika Kusini aliuawa na majangili Desemba mwaka 2012.
Kwa mujibu wa Naibu
Waziri huyo, baada ya kupokea taarifa, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na
Utalii, kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ilichukua hatua ya
dharura kuagiza msako wa majangili katika maeneo yote yanayozunguka hifadhi
hizo mbili.
“Serikali inawasaka kwa
udi na uvumba raia hao watatu na wananchi wanaombwa kusaidia kutoa taarifa kwa
vyombo vya ulinzi na usalama, sambamba na hatua hiyo, mapema leo (jana), wizara
imetuma kikosi maalum (Rapid response team) cha askari 20 wakiwa na silaha na
vifaa maalumu ili kuongeza nguvu na kuhakikisha majangili wanapatikana,”
alieleza Nyalandu.
Akielezea hatua
nyingine zilizochukuliwa katika mapambano dhidi ya ujangili, Nyalandu alisema
serikali katika kutekeleza maazimio ya Bunge yaliyotolewa na Kamati ya James
Lembeli, Mbunge wa Kahama (CCM), imechukua hatua mahususi ikiwa ni pamoja na
kutekeleza agizo la Rais Kikwete la kuundwa kwa Tume ya Kimahakama kuchunguza
tuhuma dhidi ya operesheni tokomeza.
Nyalandu alisema baada
ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika operesheni hiyo, serikali
itaendesha operesheni nyingine. Lakini wakati ikijiandaa kwa `vita’ nyingine
kali dhidi ya majangili, alisema wizara imewasimamisha kazi watumishi 23
wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali zikiwemo za kula rushwa na kusaidia majangili.
Alisema pamoja na
taarifa za kukamatwa kwa meno ya tembo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo
tukio lililoripotiwa katika Bandari ya Dar es Salaam mapema mwezi huu, wiki
iliyopita, katika Kijiji cha Ugenza, Mufindi, waliwakamata majangili watatu wakazi
wa Dar es Salaam wakisafirisha meno ya tembo kilo 37.
Aliwataja waliokamatwa
na maeneo wanakoishi kwenye mabano kuwa ni mwanamke mmoja ambaye ni Salome
Aloyce (Sinza Madukani), Rajabu Omari (Kigogo) na Kadili Kisanduku (dereva
teksi wa Mbezi Louis). Alisema walikuwa na gari aina ya Toyota Corona yenye
namba za usajili T580 ABL, mali ya Florian Elias wa Dar es Salaam na walikuwa
wanaelekea jijini humo. Sasa wanashikiliwa na Polisi.
Katika kipindi cha
miaka mitatu (2008 hadi 2013), meno ya tembo yenye uzito wa kilo 32,987
yalikamatwa ndani na nje ya nchi, jambo lililo ishara ya kukithiri wa ujangili
wa wanyama hao nchini.
Mwaka 2010, Tanzania
ilipigiwa mstari mwekundu kuwa moja ya nchi iliyoathirika zaidi kwa ujangili na
biashara ya meno ya tembo duniani. Idadi ya tembo inaelezwa kupungua nchini kwa
kasi ambapo mwaka 2009 kulikuwa na tembo 109,000 lakini kutokana na ujangili,
walifikia 70,000 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment