Winnie Mandela. |
Chifu wa ukoo huo anaotoka Mandela, Daludumo Mtirara alisema juzi jioni kuwa ukoo huo umekataa kumtambua Makaziwe na badala yake utaendelea kumtambua mjukuu wa Mandela, Mandla kuwa Mkuu wa familia.
"Winnie amepotosha umma kuhusu utamaduni wa ukoo wa kichifu wa AbaThembu," alisema Mtirara.
Chifu huyo alisema miaka sita iliyopita, Mandela mwenyewe alimtangaza Mandla kuwa Mkuu wa familia na alikabidhiwa silaha ya kichifu.
Jumatano iliyopita Winnie alielezea kutofurahishwa na namna vyombo vya habari vinavyoripoti taarifa kutoka katika familia ya kiongozi huyo.
Msemaji wa Winnie, Thato Mmereki alisema kwa kufuata utaratibu wa utamaduni wa familia hiyo, mtoto mkubwa wa kike wa Mandela, Makaziwe, atakuwa Mkuu wa familia na atashirikiana na wadogo zake wa kike wawili, Zenani na Zindziswa kufanya uamuzi.
Msimamo huo wa Winnie ulitangazwa siku chache baada ya kuripotiwa kuibuka upya kwa ugomvi kati ya watoto na wajukuu wa shujaa huyo wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi duniani.
Inadaiwa siku chache kabla ya maziko ya Mandela, Mandla alifukuzwa katika nyumba ya babu yake katika kijiji cha Qunu.
Mbali na kufukuzwa, inadaiwa vitasa vya nyumba hiyo vilibadilishwa na huduma za maji na umeme zilizokuwa zikitumika katika nyumba ya Mandla kijijini hapo, zilisitishwa.
Hata usafiri kwa ajili ya kwenda mazikoni haukutolewa kwa ndugu waliozaliwa pamoja na Mandla na wanasiasa na viongozi wa dini waliokuwa wakishirikiana na mjukuu huyo, walitengwa na wengine kukosa mwaliko wa kuhudhuria maziko ya Jumapili.
Inadaiwa kwamba Makaziwe, alimtaka Mandla, ambaye ni Chifu wa Mvezo, kijiji alichozaliwa Mandela, kutoa mifugo yake iliyokuwa katika eneo la nyumba hiyo.
Gazeti la The Times, lilibainisha kwamba mjane wa Mandela, Graca Machel na mwanasheria wa siku nyingi wa kiongozi huyo, George Bizos, walijaribu kuwataka wanafamilia hao kudhibiti hali hiyo isijioneshe lakini bila mafanikio.
Ugomvi huo unatajwa kutokana na mgogoro ulioibuka wakati Mandela akiwa mahututi katika Hospitali ya Med Clinic, kuhusu wapi alipaswa kuzikwa kati ya kijiji alichozaliwa cha Mvezo au alichokulia cha Qunu.
Wosia wa Mandela uliofunguliwa akiwa katika hospitali hiyo ya Pretoria, ulieleza wazi kuwa alipenda azikwe karibu na wanawe walikozikwa na kwa wakati huo, makaburi yao yalikuwa Mvezo.
Wanawe hao, Makgato aliyefariki dunia mwaka 2005; Makaziwe, ambaye ni mwanawe wa kike wa kwanza aliyefariki dunia akiwa mchanga mwaka 1948; na Madiba Thembekilea, aliyekufa kwa ajali ya gari mwaka 1969; walizikwa Qunu.
Hata hivyo, Mandla, ambaye ni mtoto wa Makgato na Mbunge kwa tiketi ya ANC, alifukua miili hiyo mwaka 2011 na kuizika upya Mvezo, alikozaliwa babu yake.
Uamuzi huo wa Mandla ambao haukushirikisha familia, ulisababisha watoto wa Mandela, wakiwakilishwa na mwanasheria, Sandla Zigadla, kwenda mahakamani kutaka mabaki ya ndugu zao, yarudishwe Qunu.
Jaji Lusindiso Pakade, alitoa amri kumtaka Mandla aache kuingilia mchakato wa kuhamisha mabaki ya miili hiyo kutoka Mvezo kwenda Qunu.
Mandla alifanya jaribio la kuzuia mchakato huo, lakini Jaji Pakade, alizuia jaribio hilo na badala yake akakazia hukumu kutaka miili hiyo ifukuliwe haraka.
Baada ya hukumu hiyo, huku vyombo vya habari vya Afrika Kusini na kimataifa vikishuhudia, maofisa wa Serikali walivunja lango la makazi ya Mandla kwa vifaa maalumu, ili kutoa nafasi kwa gari la kubeba maiti kuingia ndani yalikokuwa makaburi hayo.
Miili ilifukuliwa na uchunguzi wa kisayansi kufanyika kwa takribani saa mbili na kuthibitisha kwamba ni mabaki ya watoto hao, kabla ya kuzikwa upya Qunu ambako ndiko pia Mandela alikozikwa.
No comments:
Post a Comment