Tuesday, December 3, 2013

SUMATRA KUADHIBU WALANGUZI WA NAULI MSIMU WA SIKUKUU...

Abiria katika kituo kikuu cha mabasi ya mikoani Ubungo.
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra) imejipanga kupambana na walanguzi wa nauli za mabasi katika msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.Meneja Mawasiliano kwa Umma wa Sumatra, David Mziray alisema katika taarifa yake jana kwamba   wamiliki wa mabasi watakaokiuka masharti ya leseni za usafirishaji, watachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kusimamishwa leseni ya usafirishaji.
“Baadhi ya kampuni za mabasi ya kwenda mikoani huchukua nafasi hii kuongeza nauli kiholela kwa nia ya kujinufaisha zaidi, kwenda mwendokasi, kutumia ratiba za kughushi, kutozingatia ratiba walizopewa,  kutoandaa na kutunza orodha ya abiria wanaosafiri.
“Wamiliki watakaokiuka masharti ya leseni za usafirishaji, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kusimamishwa leseni ya usafirishaji,” alisema Mziray katika taarifa hiyo.
Mwandishi alitaka kujua nauli zitakazofuatwa, ambapo Sumatra ilisisitiza kuwa nauli zinazotakiwa kutozwa ni zilizokubaliwa kisheria na kutangazwa tangu Aprili mwaka huu.
Ili kukabiliana na hujuma hizo za wakati wa siku kuu za mwisho wa mwaka, Sumatra imewataka wananchi na abiria kutoa ushirikiano kwa vyombo husika mara wanapobaini kuwepo kwa vitendo vya kuhatarisha usalama, unyanyasaji na usumbufu kwa abiria.
Sumatra kwa kushirikiana na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, imesisitiza kwa wamiliki wote wa mabasi kutekeleza masharti yote ya leseni ya usafirishaji ipasavyo.
Aidha, mabasi yatakayokutwa yamezidisha nauli, mbali na kufutiwa leseni zao za uendeshaji, pia yatatakiwa kurudishia abiria kiwango cha nauli kilichozidi na kutoa faini ya Sh 250,000.
Abiria nao wanashauriwa kupanga safari zao mapema, ikiwa ni pamoja na kukata tiketi ili kuondokana na usumbufu pamoja kulanguliwa nauli wakati wanapotaka kusafiri.

No comments: