CCM YAWAWEKA KIKAANGONI MAWAZIRI WAKE SABA...

Nape Nnauye.
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imethibitisha kuwaita na kuwahoji mawaziri saba wa Rais Jakaya Kikwete kutokana na mambo mbalimbali yaliyoibuliwa kwenye ziara za Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana katika mikoa ya Ruvuma na Mbeya hivi karibuni.
Hayo yamethibitishwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliyesema jana jijini Dar es Salaam kuwa, mawaziri hao walihojiwa katika kikao kilichofanyika juzi mjini Dodoma.
Aliwataja mawaziri hao kuwa ni Christopher Chiza Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Shukuru Kawambwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Celina Kombani Waziri wa Utumishi na Hawa Ghasia Waziri wa TAMISEMI.
Wengine ni Dk Abdallah Kigoda Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Mathayo David Mathayo - Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Saada Mkuya- Naibu Waziri wa Fedha aliyejieleza kwa niaba ya Waziri wa Fedha.
Alisema baada ya maelezo ya kutosha kutoka kwa mawaziri husika, Kamati Kuu imetoa ushauri wake kwa Rais juu ya mawaziri hao, lakini akashindwa kuueleza msimamo huo kwa madai kuwa, kuuanika kwa umma itakuwa sawa na kutoa amri kwa Rais  ambaye kwa nguvu aliyonayo kisheria, ndiye atakayekuwa na uamuzi wa mwisho juu ya alichoshauriwa.
Aidha alisema kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Kikwete pamoja na mambo mengine ilipokea taarifa ya ziara ya Kinana na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti kwenye baadhi ya mikoa nchini.
Alisema, Kuhusu wakulima wa pamba kamati hiyo imeiagiza Serikali iangalie upya upatikanaji wa pembejeo za ruzuku kwa wakulima wa pamba nchini.
Aidha alisema uwepo wa mbegu bora ni muhimu, lakini ni vizuri pakawa na ushindani unaozingatia ubora ili kuondoa ukiritimba wa mtengenezaji mmoja, hivyo kusaidia bei kuwa nzuri kwa wakulima.
"Hata hivyo Chama kimeiagiza Serikali kutowalazimisha wakulima kutumia mbegu ya Quiton badala yake elimu itumike zaidi badala ya nguvu. Pia iangalie upya utaratibu wa kutoza bei ya mbegu ya Quiton kwa dola za Kimarekani badala ya pesa ya Kitanzania, wakizingatia mbegu hiyo inazalishwa nchini," alisema.
Alisema Kamati Kuu pia imepongeza juhudi za Serikali kuvutia wawekezaji kwenye viwanda vya pamba mjini Shinyanga, hata hivyo imeitaka Serikali kuangalia upya urasimu katika uwekezaji wa viwanda nchini hasa vinavyoongeza thamani ya mazao na kutoa ajira nyingi nchini. Aidha alisema Kamati imetaka wakulima wasilazimishwe kufanya kilimo cha mkataba bali waingie kwa hiari yao wenyewe.
Kuhusu wakulima wa korosho Kamati hiyo imesema pamoja na kuridhishwa na hatua za muda mfupi kwa msimu wa korosho kwa mwaka 2013/2014 ambazo zimesaidia bei na soko kuwa afadhali, bado imesisitiza Serikali kujipanga kutatua tatizo la korosho kwa suluhisho la kudumu kwa kuhakikisha korosho inabanguliwa nchini.
Pia imetaka Serikali kuangalia upya orodha ndefu ya makato wanayokatwa wakulima hasa wa korosho na vyama vya msingi au mamlaka zinginezo ili kuondoa makato yasiyo ya lazima ili kuongeza kipato cha mkulima.
Kuhusu pembejeo za ruzuku, Kamati Kuu imepokea taarifa ya malalamiko ya wakulima juu ya ufanyaji kazi wa mbolea ya minjingu na kuagiza kuwa pamoja na kuendelea na utafiti wa nini kinachotokea kwenye mbolea hiyo ya minjingu kiasi cha kuleta malalamiko yote hayo, wananchi wawe huru kutumia mbolea wanayoitaka badala ya kulazimishwa kutumia mbolea wanayoilalamikia ya Minjingu.
"Serikali iangalie utaratibu bora wa kuratibu swala zima la pembejeo za ruzuku ili lifaidishe zaidi wakulima walio wengi badala ya utaratibu wa sasa ambao licha ya kulalamikiwa na wakulima unaotoa mwanya kwa watu wachache kutumia vibaya utaratibu huo kuiibia Serikali na wakulima," alisema.
Akizungumzia madai ya walimu, Kamati Kuu imesisitiza kupandishwa vyeo na kulipwa stahiki  zao walimu ni haki yao ya msingi hivyo lazima itekelezwe bila kuwa na visingizio na ifanyike kwa haki.
Aidha, alisema unaangaliwa utaratibu wa kuboresha mawasiliano kati ya wizara zinazohusika na kusimamia walimu, Kamati Kuu imeitaka Serikali jambo hili lifanyike mapema ili kupunguza malalamiko ya walimu.
Aidha Kamati Kuu imeitaka Serikali na wabunge wa CCM kuzijadili kwa makini ripoti hizo na kufikia hitimisho la migogoro hii nchini. 
Hata hivyo, Kamati Kuu imeitaka Serikali kuangalia upya utaratibu uliotumika kuwamilikisha watu wachache maeneo makubwa ya ardhi, ambao wameshindwa kuyaendeleza badala yake wanayatumia kuwakodishia wakulima wadogo.
Aidha alisema maagizo yote haya yatatolewa taarifa kwenye Chama mara kwa mara, ili kukiwezesha chama kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010/2015.
Wakati Kamati Kuu ya CCM ikiwabana mawaziri wake ili waendane na kasi ya ilani ya chama hicho tawala, mwandishi wetu Halima Mlacha anaripoti kutoka Dodoma kuwa, wabunge wameungana kwa sauti moja na kuhoji kwanini sekta ya afya haijaingizwa kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) wakati sekta hiyo ni moja ya injini za maendeleo.
Pia wabunge hao, wakiwemo wa CCM walipendekeza kuunganisha nguvu za wabunge na kuwang’oa mawaziri wanaoshindwa kuwajibika kila Kamati za Bunge zinapowasilisha ripoti zao za mwaka.
Wabunge hao waliyasema hayo wakati wakichangia, mijadala ya taarifa zilizowasilishwa za Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Maendeleo ya Jamii.
Akichangia mjadala huo, Lusinde, pamoja na kutaka mawaziri wawajibishwe na wabunge, pia alilaumu ni kwanini hadi sasa sekta hiyo ya afya haipo kwenye mpango huo wa BRN.
“Ili uchumi ukue unahitaji taifa lenye afya, nimeshangazwa sana kuona sekta hii Serikali haijaona umuhimu wake,” alisema.
Mpango huo wa BRN umejumuisha sekta sita ambazo ni gesi asilia, kilimo, maji, elimu, uchukuzi na matumizi ya rasilimali.
Pamoja hayo Lusinde aliwashangaa wabunge waliokuwa wakisimama na kutamka kwamba mawaziri wasijiuzulu.
“Sisi kama wabunge tunachotaka ni kuona matokeo mazuri, iwapo ripoti hizi zinaibua mambo makubwa, lazima tukubaliane kuwaondoa hawa mawaziri. Hata uwanjani kocha hujiuzulu pale timu inapofanya vibaya wakati hachezi,” alisisitiza Lusinde.
Alisema kwa bahati nzuri Bunge hilo, lilimpeleka China kwa ajili ya kujifunza ambapo alibaini kuwa mawaziri nchini humo hali zao kiafya hudhoofika wakati wa Bunge kutokana na kazi kubwa wanayofanya.
“Sisi hapa mawaziri wanazidi kunenepa, unawaona wanaingia katika Facebook, hivi mtu unapata wapi nafasi ya kuingia kwenye Facebook wakati Bunge linakutana ni vichekesho vikubwa sana, vitu vya ajabu sana,” alisema.
Alisema ili Bunge hilo liweze kuheshimiwa ni lazima kuhakikisha kuwa kila taarifa ya Kamati inayowasilishwa,  watendaji wabovu wakiwemo mawaziri wanawajibishwa.
Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, aliyataka Mashirika ya Hifadhi ya Jamii, kuwaingiza kwenye mpango wa hifadhi wakulima nchini kupitia Vyama vyao vya Ushirika.
Aidha alizungumzia walimu kutopewa kipaumbele katika mishahara yao jambo linalochangia utendaji wao shuleni kushuka na kushusha sekta ya elimu nchini.

No comments: