AUAWA KWA KUKUTWA UCHI KWENYE SHIMO LA DHAHABU...

Mkazi wa Kijiji cha Kapanda  Wilaya ya Mlele  Mkoa wa Katavi, Yunge  Maboja  (70)  amekufa  baada ya kushambuliwa  na wananchi  kwa kupigwa na  silaha za jadi, ngumi na mateke  baada ya kukutwa mtupu  usiku wa manane kwenye shimo la kuchimba dhahabu.

Kwa mujibu wa blogu ya Katavi Yetu, mtu huyo aliuawa kwa kutuhumiwa kuwa  alikuwa akiroga  ili mwenye shimo hilo asipate madini ya dhahabu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi,  Dhahili Kidavashari  tukio  la kushambuliwa kwa mtu huyo, lilitokea juzi majira ya saa 7:00 usiku  katika Kijiji hicho cha Kapanda.
Alisema wiki  tatu kabla ya tukio hilo, Maboja  alimwazimisha  Idd Kipara  shoka ambalo  alikuwa akilitumia  katika shughuli  zake za ulinzi  katika shimo  la kuchimba madini ya dhahabu la Juma Ngegeshi.
Alieleza  Maboja alianza kumtafuta  mtu aliyemuazimisha  shoka  na ndipo siku hiyo ya tukio majira ya saa saba usiku,  alipofika kwenye  shimo la kuchimba dhahabu  la mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja La Abui,  ambapo alichungulia ndani ya shimo , ambalo  ndani yake walikuwemo watu wawili wakifanya shughuli hizo za uchimbaji wa  madini.
Kidavashari  alisema  watu hao waliokuwa ndani ya shimo  walishitushwa  na kitendo cha Maboja, kuwachungulia muda huo wa usiku wa manane wakiwa ndani ya shimo hivyo iliwalazimu  watoke nje ya shimo hilo na kumkuta Maboja akiwa mtupu.
Alidai ndipo watu hao, Abui  na Hassan  walimshambulia mzee huyo  kwa fimbo na mateke  na kumlazimisha  awapeleke kwa mwenyeji wake,  Juma  Ngegeshi  ili awapatie uchawi ambao ulikuwa umebaki   uliobaki nyumbani kwake.
Alidai walipofika nyumbani  kwa Juma Ngegeshi  walimkuta  mkewe,  aitwaye  Asha  Shaban ambaye baada ya kuwafungulia mlango,  walimtaka awaoneshe uchawi  uliokuwa umebaki ndani ya nyumba hiyo na    Asha  aliwajibu ndani ya nyumba yake, hakuna kitu kama hicho.
Kauli hiyo uiliwaudhi watu hao, ambao walianza kumshambulia kwa  fimbo usoni na mgongoni na kumfanya Asha  apige yowe na badala ya kusaidiwa,  watu hao waliungana  kuanza kumshambulia mzee huyo pamoja na Asha, ambaye alifanikiwa kutoroka na kujifungia ndani.
Kidavashari alisema majeruhi wote wawili,  walifikishwa Kituo cha Polisi cha Mpanda  na kisha walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda  na mzee huyo  alikufa akiendelea kupatiwa matibabu.
Polisi wanaendelea na juhudi za  kuwasaka  wahusika  wa tukio  huku  watu wawili  wanashikiliwa  na Jeshi la Polisi kwa  mahojiano.
Watu hao ni  Yunge   Hassan (43) mkazi wa Mtaa ya Kashaulili na  Ayub Samwel (30) mkazi wa Kijiji cha Kapanda  na wengine walikimbia .

No comments: