AUA MKEWE KWA KUMCHARANGA MAPANGA BAADA YA KUDAIWA UNYUMBA...

Kamishna Dhahiri Kidavashari.
Mwanamke  mkazi  kitongoji  cha Tulieni  kijijini Tumaini  wilayani  Mlele, Rehema  Lubinza (47) ameuawa  kikatili  kwa  kucharangwa  na mapanga na mumewe  kisha  mwili  wake  kufungiwa  ndani  ya nyumba  yake  kwa  siku  tatu.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda  wa Polisi Mkoa  wa Katavi, Kamishna Dhahiri Kidavashari  alisema mauaji hayo yalifanyika mkesha wa  Sikukuu ya Krismasi , Desemba 24   katika kitongoji  hicho  cha Tulieni, Kata ya Itenka.
Kidavashari  alimtaja  mtuhumiwa  wa mauaji hayo kuwa  Mathias Mashini 'Igoka' (46)  mkazi  wa kitongoji  cha kijiji  hicho  cha Tulieni  ambaye  anadaiwa  kuishi  na  mkewe huyo  kwa miaka  mingi  bila kujaliwa  watoto.
Akisimulia  mkasa  huo Kidavashari  alidai kuwa  kwa siku  kadhaa  wanandoa hao  walikuwa    wakishutumiana  ambapo  mke alikuwa  akimshutumu  mumewe  kwa kushindwa kumpatia  mahitaji  muhimu  ukiwemo  unyumba kwa muda mrefu .
Inadaiwa kuwa  baada  ya  kuoana mke  alimkaribisha mumewe  nyumbani kwake Tulieni na kufanya makazi.
Kwa mujibu  wa Kidavashari,   mke baada ya kuona mume haeleweki  alimtaka  mumewe  huyo   atoke  nyumbani  kwake (Rehema)  kwa  madai  kuwa  ameshindwa  kumpatia mahitaji muhimu  ukiwemo unyumba  kwa muda mrefu  kauli ambazo  zilimkasirisha mume  huyo ambaye  inadaiwa hakuwa  tayari  kuachana na  mkewe.
Inadaiwa mwanamke  huyo alimfukuza mumewe huyo nyumbani  hapo  akisisitiza lazima aondoke  ndipo  mume huyo  akishirikiana na  mkazi wa  kitongoji  hicho  aliyetambuliwa  kwa jina la Ngussa Masengwa (39)  walimshambulia  mwanamke huyo  kwa mapanga  akiwa amelala  nyumbani  kwake hapo   na kumjeruhi vibaya sehemu  mbalimbali  za mwili wake na kumsababishia umauti  kisha  waliufungia mwili  wa marehemu  ndani ya  nyumba yake hiyo.
Kwa mujibu  wa  Kidavashari  Siku ya Desemba 25  majirani  baada  ya kutowaona  wanandoa hao   huku nyumba yao  ikiwa imefungwa  mchana  kutwa, waliamua kuwasiliana  na Mathias  kwa  simu  yake ya mkononi  ambaye  aliwaeleza kuwa  wako  Mpanda mjini  wakila Sikukuu  ya Krismasi .
Inadaiwa siku iliyofuata   majirani  wa  wanandoa  hao  walianza kusikia harufu  mbaya  ikitokea  ndani  ya  nyumba ya  wanandoa  hao  ndipo  walipolazimika  kuvunja   mlango  wa  nyumba  hiyo  na kushuhudia  mwili wa marehemu  ukiwa    sakafuni    chumbani  kwa   wanandoa hao ukiwa na majeraha makubwa  shingoni ,  mgongoni  na  kichwani.
Kidavashari  alisema baada ya watu hao kushuhudia hali hiyo walimpigia simu mwanamume huyo lakini hakupatikana na ndipo walipoitaarifu Polisi.
"Baada ya msako  mkali  kwa kushirikiana na  wananchi  mtuhumiwa  alikamatwa  akiwa  amejificha  wilayani Sikonge katika Mkoa  wa  jirani  wa Tabora baada ya mahojiano  na  polisi  alikiri  kutenda uhalifu  huo ambapo  alimtaja  Ngusa  kuwa  alishirikiana naye,"  alidai Kamanda  wa Polisi .
Kidavashari  aliongeza kuwa  mshtakiwa mwingine  Ngusa  alikamatwa  akiwa  anaendelea na shughuli  zake  kama kawaida  katika Kitongoji  hicho  cha Tulieni  ambapo  wote wawili  wanatarajiwa  kufikishwa mahakamani  mara tu  baada ya  uchunguzi  wa awali wa shauri  hilo  kukamilika.

No comments: