![]() |
| Philipo Mulugo. |
Mulugo alisema hayo jana wakati wa mahafali ya Chuo Kikuu cha Tumaini Kampasi ya Dar es Salaam kwenye Viwanja vya Karimjee.
Alisema dhana ya kuwepo kwa Daraja la Tano katika mfumo mpya, haikueleweka kwa wadau wengi na kwamba wataendelea kuelimisha umma juu ya mfumo huo mpya.
“Msiniulize mantiki hii ya divisheni 5 na Sifuri, kwa sababu ufafanuzi utatolewa. Kufaulu ni kufaulu tu na kufeli ni kufeli tu, hiyo divisheni 5 ni kufeli tu,” alisema Mulugo katika mahafali hayo.
Ufafanuzi wa Mulugo, umekuja siku mbili baada ya Serikali kutangaza kufuta mfumo wa zamani wa viwango vya upangaji wa alama za ufaulu kwa kidato cha nne na sita, ikielezwa kwa sasa hakutakuwa na Daraja Sifuri na badala yake kutakuwa na Daraja la Tano.
Mfumo huo umeelezwa utaanza kutumika kwa wahitimu wa kidato cha nne mwaka huu, ambao kesho wanatarajiwa kuanza mtihani wao wakati kwa kidato cha sita, utaanza mwaka kesho.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome juzi alikaririwa akiwaambia waandishi wa habari, kuwa mabadiliko hayo yanalenga kuimarisha mfumo wa elimu nchini na kuweka uwazi kwenye mitihani.
Kuanzia mwaka huu, alama 60 zitatokana na mtihani wa kidato cha nne na nyingine 40 zitatokana na mtihani wa kidato cha pili, mitihani mitatu ya mihula ya kidato cha tatu na mazoezi ya vitendo.
Kutokana na mabadiliko hayo, juzi baadhi ya wadau wa elimu nchini wameishauri Serikali kufumua mfumo mzima wa elimu badala ya kugusa vitu vidogovidogo tu.
Walitaka kurudishwa kwa somo la Siasa katika masomo ya elimu ya sekondari, ili kukabiliana na vurugu za kisiasa kwa wanasiasa wachanga.
Pia, walitaka kuanzisha masomo ya Maadili na Uzalendo, kwani lengo la wanafunzi wa sekondari si kufaulu mitihani tu.

No comments:
Post a Comment