Saturday, November 9, 2013

WABUNGE WAGOMEA MUSWADA WA KUKOMESHA MAGAZETI CHOCHEZI...

Baadhi ya magazeti yakiwa sokoni.
Bunge limegoma kupitisha marekebisho ya vifungu vya adhabu kwenye Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, ikitaka adhabu ziongezwe kwa wanaochapisha habari au kauli za uchochezi zinazovuruga amani katika jamii, na kutaka Muswada wa habari uletwe bungeni kujadiliwa.

Uamuzi huo wa bunge ulitolewa jana na bunge wakati Bunge lilikaa kama kamati ya bunge zima kupitisha marekebisho ya vifungu vya muswada wa Sheria Mbalimbali, ikiwemo hiyo iliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema .
Awali juzi wakati walichangia mjadala wa marekebisho kwenye muswada huo, wabunge mbalimbali walionesha kupinga marekebisho hayo ya adhabu na kutaka viondolewe na badala yake muswada mzima uletwe bungeni kujadiliwa.
Wabunge waliochangia kupinga kupitishwa kwa marekebisho hayo na kutaka muswada mzima uletwe bungeni kujadiliwa ni pamoja na mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM) akiungwa mkono na Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama (CCM), Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM).
Wengine ni Mbunge wa Viti Maalumu Martha Mlata(CCM), Mbunge wa Ole, Rajab Mbarou (CUF), Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (Chadema), pamoja na kambi ya upinzani bungeni  ingawa pia wengi wa wabunge waliunga mkono kwa kupiga makofi.
Akichangia Mhagama alisema jambo muhimu ni serikali ikaja na Muswada mzima na sio kuleta vifungu nusu nusu na kuhoji kwa nini serikali inapata kugugumizi kuuleta muswada huo bungeni kujadiliwa.
“Muswada wa habari ukiletwa bungeni ukajadiliwa na kupitishwa utakuwa suluhu na tutapata sheria nzuri ya kiviongoza vyombo vya habari na taaluma nzima, hivyo kwa wale watakaokiuka adhabu zinaainishwa wazi na zitawakabili.
Aliongeza  muswada  huo ndio suluhu na ukombozi wa tasnia ya habari na kwamba hata hao wachache wanaopvitumia vyombo vya habari vibaya pamoja na waandishi kwa kuisaliti nchi yao watabanwa na itabidi waandishi wazingatie sheria, lakini kuongeza adhabu tu bila kuleta sheria nzima sio suluhu.
Aidha alisema tasnia ya habari ni kama tasnia nyingine lakini hivi sasa wapo wachache wanaoidhalilisha kwa maslahi yao, lakini ikiwepo sheria itawalinda na pia itawaongoza nini cha kufanya na kipi hakitakiwi.
“Mimi ni Mwenyekiti kamati ya Jamii, Bunge lilitupeleka India kujifunza namna gani tunaweza kutengeneza sheria nzuri ya tasnia hii, lakini tukiangalia tu vipengele viwili vya adhabu sio kikwazo pekee kwenye nchi yetu lazima tuangalie sheria mzima, alisema Mhagama.
Na kuongeza, anakubali kwamba wapo waandishi wasio na nidhamu lakini kuongeza adhabu bila kuwa na sheria bora hakutatatua tatizo na kwamba kamati iliwahoji mawaziri tofauti waliowahi kuongoza wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na wao kukiri kwamba Muswada wa habari upo tayari.
“Nakubali kabisa wapo waandishi wasio na nidhamu, lakini kamati tumehoji wizara wamesema  muswada  uko tayari tangu mwaka 2006, tunang’ang’ania kuleta kifungu kidogo cha adhabu, Mkuchika (wakati huo akiwa Waziri husika), alionesha ushirikiano , akaja Nchimbi naye akasema muswada uko  tayari, sasa yupo Dk Fenella Mukangara naye amesema uko tayari, sasa kwanini tusiulete?, tunapata kigugumizi gani, alihoji Mhagama.
Na kusema wabunge wakiuondoa kwenye bunge hili, Bunge lijalo la Desemba serikali itaona umuhimu wa kuuleta na hivyo kujadiliwa na kisha kupitishwa kuwa sheria ya habari itakayoangalia pia maslahi ya wanahabari.
Akichangia hoja hiyo mjadala huo Serukamba alisema anawaomba wabunge  kwa pamoja wakubaliane na yeye kwenye hoja hiyo kupinga marekebisho ya sheria hiyo ili serikali ilete muswada huo bungeni kujadiliwa.
“Kwa nini kuna haraka ya kuleta marekebisho ya adhabu, badala ya kuleta Muswada wa habari, ni vyema muswada wa habari ukaletwa hapa, ili tutunge sheria itakayoongoza sekta hii, na hizo adhabu hata zikiongezwa mimi sitapinga, ili mradi tutakuwa tumepitisha sheria”, alisema Serukamba.
Katika, hatua nyingine alisema uchochezi haufanywi tu na vyombo vya habari bali pia unatengenezwa na wanasiasa wenyewe na kwamba sheria ikiwepo itatoa mwongozo na atakayekiuka atakabiliwa na adhabu.
Hata hivyo baada ya hoja mbalimbali bunge kama kamati likawahoji wabunge wanaokubali au kukataa mapendekezo hayo ya serikali, ambao wengi wao walipinga na hivyo serikali ikatakiwa kuleta muswada bungeni.
Hata hivyo baada ya marekebisho hayo kuondolewa kwa wabunge kupinga, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema, alisimama na kuomba kura zihesabiwe, jambo ambalo Spika alisimama na kusema ni katika jambo hilo halina utani wa sheria na kwamba ni muda mrefu sasa serikali haijaleta muswada huo na kutaka uletwe kujadiliwa na Bunge.
“Mheshimiwa Mukangara, tunataka sheria, hata mimi mimi nataka hiyo sheria, ni kweli  imechukua muda mrefu sana”, aliunga mkono Spika.
Katika sheria hiyo, serikali ilileta mabadiliko ya kifungu cha 36 (1) na 37 (1) (a) ambapo vimeongeza adhabu ya faini kutoka shilingi 150,000 hadi kufikia Sh milioni tano kwa watenda kosa la uchochezi wa kutumia lugha unaoweza kusababisha kuvunjika kwa amani nchini.
Au kutumikia adhabu ya miaka mitatu jela, au vyote kwa pamoja.
Awali akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani bungeni juzi, msemaji wa kambi hiyo,Tundu Lissu aliitaka serikali kufuta kabisa sheria ya magazeti ya sasa na badala yake ilete Muswada wa habari Bungeni, utakaotunga sheria mpya .
Lissu alisema hiyo inatokana na ukweli kwamba kuna madai ya msingi ya muda mrefu yaliyotolewa mwaka 1991 na Tume ya Nyalali ikitoa mapendekeo kwa serikali kuelta sheria ya uhuru wa magazeti kwani sheria zilizopo hazitoi uhuru kwenye vyombo hivyo.
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala Dk Pindi Chana aliwaomba wabunge, wahariri na wadau wa masuala ya habari nchini kumpa majibu ya maswali pale ambapo magazeti yanatumika kupendelea upande mmoja au kuvuruga amani, nini kifanyike, kwani huko ndiko uhuru wa habari, alihoji Dk Pinda.
Hata hivyo pamoja na marekebisho ya sheria hiyo kupingwa Muswada wa marekebisho ya Sheria mbalimbali ulipitishwa.

No comments: