SOKO KUU LA KARIAKOO LAKOSA MWEKEZAJI MWENYE VIWANGO...

Sehemu ya nje ya Soko Kuu la Kariakoo, Dar es Salaam.
Uongozi wa soko la Kariakoo, umesema haujapata mwekezaji mwenye vigezo atakayejenga upya soko dogo na kuwa la kisasa.

Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi jana Mkurugenzi wa soko hilo, Florens Seiya, alisema mwekezaji aliyepatikana awali hakufikia vigezo vinavyotakiwa, hivyo kukataliwa.
Seiya alisema Kituo cha Uwekezaji (TIC), kilimkataa mwekezaji huyo kwa madai ya kutokidhi viwango vinavyotakiwa na kituo hicho na wanatafuta mwekezaji mwingine.
"Alikuwa amepatikana mwekezaji ambaye alikuwa tayari, lakini wenzetu wa TIC wakasema hajafikia viwango vinavyotakiwa, vile vile kuna wawekezaji wengine lakini bado nao hawana viwango," alisema Seiya.
Alisema soko hilo linatakiwa kuwa la kisasa ambamo huduma zote zitapatikana, hivyo kuhitajika mwekezaji mwenye viwango stahiki.
Aidha, Seiya aliongeza kuwa hali ya biashara si mbaya, na wanajitahidi kuboresha soko hilo ili lirudi katika hali ya zamani.
Soko hilo limekuwa likipoteza umaarufu kutokana na wafanyabiashara kulikimbia na kuhamia masoko mengine.
Hata hivyo, mbinu kadhaa zimeanzishwa kuhakikisha heshima  inarudi na tayari uongozi umefungua mtandao wa soko ambao utakuwa unawarahisishia wafanyabiashara kununua na kuuza bidhaa zao.

No comments: