![]() |
| Shekhe Ponda Issa Ponda. |
Hata hivyo, Shekhe Ponda naye alijikuta akiwa mahakamani hapo tangu saa nne asubuhi, baada ya kuletwa na basi la Magereza chini ya ulinzi wa askari Polisi na askari Magereza, lakini bila Wakili wake, Juma Nassoro, anayemtetea kwenye kesi hiyo.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mary Moyo ambaye amechukua nafasi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama Mkoa, Richard Kabate aliyehamishiwa kikazi mkoani Dodoma, kabla ya kuanza kusikiliza kesi hiyo, alimwuliza Shekhe Ponda kuhusu wakili wake na yeye alijibu hakuwa na taarifa zozote kuhusu wakili huyo.
Akitoa maelezo ya awali Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo , alisema kesi hiyo imefika hapo kwa ajili ya kuanza kusikilizwa na kuuliza upande wa mashitaka iwapo umeleta mashahidi wake.
Upande wa mashikata ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali , Sunday Hyera akisaidiana na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Zabron Msusi, walimfahamisha hakimu kuwa walimleta shahidi wa kwanza, askari Kingazi kwa ajili ya kutoa ushahidi upande wa Jamhuri.
Hata hivyo, hakimu huyo alisema asingeweza kuanza kusikiliza kesi hiyo, kwa vile jadala halisi la kesi hiyo, liliitishwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam tangu Oktoba 15, mwaka huu na bado lilikuwa halijarejeshwa mahakamani hapo.
Alisema kesi hiyo itaanza kusikilizwa iwapo jadala halisi, lililopelekwa Mahakama Kuu kupitiwa na Jaji, litarudishwa na kwa sasa itakuwa ikitajwa tu mahakamani hapo.
Hakimu huyo aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 21, mwaka huu itakapofikishwa tena mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa ;na aliamuru Shekhe Ponda arudishwe rumande.
Mahakamani hapakuwa na wafuasi wake wengi, kama ilivyo kawaida ya siku za kesi hiyo, kwani baadhi yao walidhani kuwa Shekhe Ponda asingeletwa mahakamani jana, kwa madai yao kuwa kuna kesi nyingine ya rufaa Mahakama Kuu, Dar es Salaam.
Mara ya mwisho kesi hiyo kufikishwa mahakamani hapo ilikuwa Oktoba mosi mwaka huu, Wakili Nassoro aliwakilishwa na Wakili Yahya Njama, aliyeiambia Mahakama kuwa Nossoro alienda nchini India kwa matibabu ya macho na anatarajiwa kurejea Oktoba 25, mwaka huu baada ya afya yake kutengemaa.
Ponda amefunguliwa kesi namba 128/2013 katika mahakama hiyo na anakabiliwa na mashitaka matatu, anayodaiwa kuyatenda Agosti 10, mwaka huu, eneo la Kiwanja cha Ndege katika Manispaa ya Morogoro.
Kosa la kwanza anadaiwa kusema: “Ndugu Waislamu msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti, kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata (Baraza la Waislamu Tanzania) ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali.
“Kama watajitokeza kwenu watu hao na wakajitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya misikiti yenu na muwapige sana.”
Kauli hiyo inadaiwa iliumiza imani za watu wengine, na kwamba ni kinyume cha hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam iliyotolewa na Hakimu Nongwa, Mei 9, mwaka huu. Hukumu hiyo ilimtaka ndani ya mwaka mzima kuhubiri amani.
Katika shitaka la pili, Shehe Ponda anadaiwa kuwa Agosti 10 mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, mshitakiwa alitoa maneno yenye nia ya kuumiza imani nyingine za dini.
Maneno hayo anayodaiwa kusema ni: "Serikali ilipeleka Jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka, na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu.
“Lakini Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristu."

No comments:
Post a Comment