Tuesday, November 5, 2013

SERIKALI YAREJESHA DIVISHENI ZIRO MITIHANI YA KIDATO CHA NNE...

Baadhi ya wanafunzi wakifanya mitihani ya Kidato cha Nne.
Serikali imerejesha daraja sifuri katika matokeo ya kidato cha nne, baada ya kutangazwa hivi karibuni kuondolewa na kuanzishwa daraja mbadala la tano.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema jana kwamba si kweli kuwa Serikali imefuta daraja la sifuri  katika mitihani ya kidato cha nne.
“Serikali haijafuta daraja sifuri na wala hakuna daraja la tano, lipo daraja la kwanza, la pili, la tatu, la nne na sifuri kama kawaida,” alisema.
Mulugo alitoa kauli hiyo, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM), aliyetaka kujua kama uamuzi wa Serikali wa kushusha madaraja katika mitihani ya kidato cha nne, lengo lake ni kuokoa wanafunzi wanaofeli.
Hata hivyo, Mulugo alifafanua, kwamba uamuzi wa kushusha madaraja, haukuwa na lengo la kuokoa wanafunzi wanaofeli, bali kuondoa mlundikano wa alama katika daraja moja.
Alisema Serikali imeweka madaraja mapya kwa kutofautisha alama kumi kumi kutoka daraja moja kwenda lingine, na kwamba   alama za ufaulu bado zinaanzia 41, ambazo ni daraja la C.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, alipokuwa akitangaza  mabadiliko katika sekta ya elimu hivi karibuni, alisema daraja sifuri limefutwa na limeanzishwa daraja la tano.
Katika mabadiliko hayo, alama za ufaulu zimeshuka ikilinganishwa na alama zilizokuwa zikitumiwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) awali.
Kwa mujibu wa alama zilizokuwa zikitumiwa na Necta za A, B, C, D na F, alama A ilianzia asilimia 81 mpaka 100, B (61- 80), C (41-60), D (21- 40) na F (0- 20).
Mabadiliko yaliyotangazwa na Profesa Mchome ambayo yamekanushwa na Mulugo, A imeshuka ambapo inaanzia asilimia (75- 100), B+ imeongezwa lakini nayo imeshuka na kuanzia asilimia 60 mpaka 74, B ya sasa (50-59).
Alama C nayo itakuwa dhaifu (40-49), D dhaifu (30-39), E ambayo ni alama mpya iliyoanzishwa (20-29) na F itaanzia (0-19).
Mabadiliko ambayo hayakukanushwa ni pamoja na utaratibu wa namna mwanafunzi atakavyopata asilimia 40 ya mtihani wake wa mwisho, kutokana na kazi atakazokuwa akifanya kuanzia alivyoingia sekondari.
Kwa kidato cha nne, asilimia 15 kati ya 40, mwanafunzi atatakiwa azipate katika mtihani wa Taifa wa kidato cha pili.
Matokeo ya mtihani wa kidato cha tatu, katika mihula yote miwili, mwanafunzi atatakiwa apate asilimia 10, kila muhula alama tano.
Mtihani wa moko kwa kidato cha nne, mwanafunzi atatakiwa kupata asilimia 10 na kazi za mradi alama tano.
Kutokana na mkanganyiko huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliagiza mabadiliko hayo yapelekwe bungeni, ili kuondoa utata.
“Nataka Waziri akae aandae kauli ya Serikali na mtuletee kauli ya Serikali kuhusu utaratibu huo ili tupate majibu ya kuridhisha,” alisema Spika.

No comments: