Friday, November 29, 2013

POLISI SASA KUTUMIKA KUFUNGA VYUO 'BUBU' VYA UFUNDI...

Philipo Mulugo.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, amesema ataanza kutumia Jeshi la Polisi, kufunga vyuo vyote vinavyoendeshwa bila ithibati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte).

Alisema hayo jana alipokuwa akifungua mkutano wa kitaifa wa wakuu wa vyuo vya ufundi nchini ulioandaliwa na  Nacte jijini hapa.
“Siku hizi kumeibuka wimbi kubwa la vyuo holela vinavyoendeshwa pasipo kuzingatia vigezo vilivyowekwa na Nacte.
“Jamii yetu imeendelea kuhujumiwa na watu wanaojitafutia fedha kwa njia za mkato na hasa wanaojitangaza kutoa elimu ya ufundi tena kwa ada ndogo,” alisema Mulugo.
Alisema kuanzia mwaka wa masomo 2014/15 ,vyuo vyote vya ufundi nchini vitaendesha mafunzo ya kozi zenye ithibati tu ili kuondoa usumbufu kwa wahitimu.
Pia alitangaza rasmi kuanza kwa mtaala wa Stashahada ya Elimu ya Msingi, ambayo itaanza kutekelezwa kwa vyuo vilivyo na sifa kuanzia mwaka wa masomo wa 2014/15.
Aliasa wazazi na walezi kabla ya kupeleka watoto wao kujiunga na vyuo vya ufundi, wahoji mambo muhimu ikiwa ni pamoja na usajili wa vyuo hivyo na taaluma za wakufunzi wake ili wawe na uhakika na taaluma inayotolewa kwa watoto wao.
“Mkikutana na vikwazo katika kutekeleza agizo langu, basi ofisi yangu ambayo ni Mamlaka ya Rufaa kwa mujibu wa sheria yenu itatoa ushirikiano kuhakikisha tatizo la kozi zisizotambuliwa linadhibitiwa kwa nguvu zote,” alisema.
Alisema kabla ya kuanzishwa Nacte, Serikali haikuwa na chombo mahususi cha kuratibu elimu na mafunzo ya ufundi, hali ambayo ilisababisha kila mwenye chuo kujiwekea vigezo na viwango vyake vya taaluma na kusababisha nchi kuwa na vyuo ambavyo vinatoa tuzo ambazo vigezo vyao havilingani.
“Kila mwenye chuo alikuwa akitayarisha mtaala wake wa mafunzo kama alivyoona inafaa, na hivyo kusababisha utofauti wa viwango vya tuzo zinazotolewa baina ya chuo kimoja na kingine,” alisema.
Alisema katika mfumo wa soko huria na kutokana na kiu ya Watanzania kupata elimu ya ufundi, ilikuwa rahisi kudanganywa na kupewa elimu duni na pia ilikuwa vigumu kwa Serikali kuweka mikakati ya kuendeleza elimu ya ufundi ili kukidhi mahitaji ya maendeleo ya nchi na watu wake.
Katibu Mtendaji wa Nacte, Dk Primus Nkwera, alivitaka vyuo na taasisi za elimu za ufundi nchini zinazotoa mafunzo bila kusajiliwa na wenye nia ya kuanzisha vyuo vipya, kuhakikisha vyuo vyao vinapata usajili wa Baraza hilo kwa mujibu wa sheria.
Mwenyekiti wa NACTE, Steven Malote, alisema Baraza hilo limeweka mfumo wa Tuzo za Kitaifa za Elimu ya Ufundi ambazo zimeunganishwa na Tuzo za Kitaifa za Ufundi Stadi (NVA), ili kuwa na ngazi 10 za Mfumo wa Kitaifa wa Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi (TVET).

No comments: