Friday, November 22, 2013

OMBI LA BABU SEYA, PAPII KOCHA LATUPILIWA MBALI, SASA 'KUFIA' JELA...

Nguza Viking 'Babu Seya' (kushoto) na mwanawe Johnson 'Papii Kocha'.
Ndugu na jamaa wakilia kwa uchungu mahakamani mara baada ya hukumu kutolewa jana.
Mahakama ya Rufani Tanzania, imetupilia mbali ombi la mwanamuziki maarufu nchini mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Nguza Viking 'Babu Seya' na mwanawe Johnson 'Papii Kocha', na kuamuru waendelee kutumikia kifungo cha maisha jela.

Uamuzi huo ulitolewa jana baada ya jopo la majaji watatu kufanya marejeo ya hukumu iliyowatia hatiani wanamuziki hao mwaka 2010.
Akisoma uamuzi huo jana, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Zahra Maruma, alisema baada ya kupitia hoja za wanamuziki hao, Mahakama imeona hazina msingi kisheria.
Alisema hoja ambazo wanamuziki hao walizitoa katika ombi lao, hazioneshi upungufu wowote katika hukumu iliyotolewa awali na Mahakama hiyo.
Kwa mujibu wa Zahra, hoja hizo zililenga kufungua upya rufaa ambayo ilishasikilizwa na kukataliwa na pia hawakueleza makosa yaliyosababisha haki kutotendeka.
Baada ya uamuzi huo, Papii Kocha akiondoka katika eneo la Mahakama alisema hakuna wa kusaidia zaidi ya Rais Jakaya Kikwete.
"Kwa hatua iliyofikia sasa tunaomba Rais atusaidie, kama kweli tulifanya Mwenyezi Mungu atatuhukumu," alisema Papii Kocha.
Wakizungumza nje ya Mahakama, baadhi ya wasanii walikuwa   eneo hilo akiwemo Jose Mara wa kundi la Mapacha Watatu, alidai walitarajia wangekuwa na wanamuziki wenzao lakini wanamshukuru Mungu kwa yote na watauenzi muziki wao.
Kwa upande wake, shemeji wa Papii Kocha, Saada Omary alidai walipata matumaini ya kumwona tena Papii, lakini imeshindikana na ingawa Mahakama ndiyo yenye mamlaka ya mwisho, wanamwomba Rais Kikwete awasaidie, kwani wameteseka sana.
Wakili wa wanamuziki hao, Gabriel Mnyele, alisema kutokana na uamuzi huo kuna umuhimu wa kuwa na Mahakama ya Juu zaidi ambayo ingewasikiliza.
Nje ya Mahakama baadhi ya ndugu na marafiki waliangua kilio, huku wengine wakiwaaga wanamuziki hao wakati wakirudishwa jela kuendelea na kifungo chao.
Babu Seya na Papii Kocha, walianza kutumikia kifungo hicho Juni 25, 2004, baada ya kukutwa na hatia ya kunajisi na kulawiti watoto.
Katika hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  Addy Lyamuya aliwahukumu kifungo hicho  Babu Seya, Papii Kocha, Nguza Mbangu na Francis Nguza baada ya kuwakuta na hatia ya makosa 23 ya kunajisi na kulawiti.
Baada ya hukumu hiyo, Babu Seya na wanawe walikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ambapo Jaji Thomas Mihayo (mstaafu), aliwatia hatiani tena na kuunga mkono hukumu ya Mahakama ya Kisutu.
Hata hivyo, Babu Seya na wanawe hawakuridhika na uamuzi huo na kwenda Mahakama ya Rufaa, ambako hukumu ilibadilika kidogo kwa Mbangu na Francis kuachiwa huru, huku Babu Seya na Papii Kocha wakibaki na hatia na kuendelea kutumikia kifungo hicho.
Kwa mujibu wa hukumu ya jana, Mahakama iliridhika na ushahidi ulio kwenye kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo kwa kila kosa na kuwaona Babu Seya na Papii Kocha, wahusika wa kutenda makosa yanayowakabili.
Katika hukumu hiyo, utetezi kwamba washitakiwa hawakuwa katika eneo la tukio, ulikataliwa. Katika hukumu hiyo, Babu Seya alitiwa hatiani kwa makosa matano ya kunajisi na Papii Kocha mawili.

No comments: