Saturday, November 16, 2013

MAOFISA WA TRA, BANDARI WATIWA MBARONI KWA MENO YA TEMBO...

Sakata la shehena na meno ya tembo yaliyokamatwa katikati ya wiki hii katika bandari ya Zanzibar, eneo la Malindi, limewatia matatani maofisa kadhaa wa Serikali, wakiwemo wawili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wengine kutoka Shirika la Bandari Zanzibar.

Kwa sasa, maofisa hao wanashikiliwa na jeshi la polisi wakihojiwa kuhusiana na shehena hiyo kubwa ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh bilioni 7.4.
Hayo yamethibitishwa na Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, akisema wafanyakazi hao wa taasisi hizo zinazoshughulikia ukaguzi wa mizigo bandarini wanahojiwa ili kupata ukweli kuhusu mzigo wa makontena hayo ambayo yalipitia chini ya ukaguzi wao kabla ya kupata kibali cha kusafirishwa nje ya nchi.
"Ni kweli tunawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kusafirisha kontena likiwa na meno ya tembo wa kampuni ya Island Sea shells...lakini pia wapo wafanyakazi wawili wa taasisi zinazoshughulikia usafiri wa mizigo katika bandari ya Malindi wa TRA pamoja na Shirika la Bandari," alisema.
Hata hivyo Kamanda Ali alikataa kuwataja watu wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi ikiwemo wafanyakazi wawili wa taasisi za ukaguzi na mapato katika Bandari ya Malindi kwa madai kwamba ni mapema sana.
Jumla ya vipande vya meno ya tembo 1,021 yaliyokuwa yameshindiliwa katika magunia 95, sawa na kilo 2,910 zenye thamani ya Sh bilioni 7.4  vinashikiliwa na Jeshi la Polisi katika kontena hilo ambalo lilikuwa katika hatua za mwisho kusafirishwa  nje ya nchi kuelekea nchi za Asia.
TRA ni miongoni mwa taasisi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na kuoneshwa vidole kutokana na sakata la kontena hilo la meno ya tembo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alipozungumza na waandishi wa habari Zanzibar mara baada ya kukamatwa kwa kontena hilo Jumatano wiki hii, alisema TRA haiwezi kukwepa lawama kuhusu  suala la kontena lenye meno ya tembo kwa sababu lilifanyiwa ukaguzi na kupasishwa kabla ya kusafirishwa.
Naye Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu wa SMZ, Issa Haji Ussi Gavu alisema taasisi za ukaguzi wa kodi pamoja na bandari ya Malindi zinatakiwa kuwa makini sana katika kukagua mizigo kabla  ya kusafirishwa nje ya nchi.
Alisema kilichofanyika katika kontena lililokutwa shehena ya meno ya tembo ni mchezo ambao umefanywa kwa ushirikiano mkubwa na taasisi mbalimbali ikiwemo zinazoshunghulika na mambo ya kodi.
"Tumegundua kwamba hivi sasa zipo mbinu nyingi zinazotumika kusafirisha mizigo ambayo ni haramu ikiwemo meno ya tembo," alisema.
Alisema Shirika la Bandari linategemea kupata mashine ya kisasa itakayotambua aina ya mizigo iliyomo ndani ya makontena ikiwemo ile inayotakiwa kusafirishwa kinyume na sheria.
Kukamatwa kwa meno ya tembo huko Zanzibar kumekuja siku chache baada ya raia watatu wa China kukamatwa jijini Dar es Salaam baada ya kukutwa na meno 706 ya tembo, sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini.
Aidha, ukamataji wa meno hayo ya tembo umekuja wakati tayari serikali imetangaza kusitisha Operesheni Tokomeza Ujangili, ambayo ililenga kunusuru wanyama walio hatarini kutoweka kutokana na kuuawa katika hifadhi za taifa nchini Tanzania. Wanyama wanaolengwa zaidi na majangili kutokana na meno yao na pembe ni tembo na faru.
Matukio ya kukamatwa kwa meno ya tembo kutoka Afrika Mashariki yamekuwa yakiripotiwa kila mara. Oktoba, 20, 2012, tani nne za meno ya tembo yenye thamani ya dola milioni 3.4 za Kimarekani yalikamatwa Hong Kong, yakidaiwa kusafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.
Aidha, Agosti 16 mwaka huu polisi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata raia wa Vietnam akiwa na meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya sh milioni 18 sawa na dola zaidi ya 11,000 yakisafirishwa kwenda nje.

No comments: