Thursday, November 7, 2013

MAJAMBAZI WAMUUA MFANYAKAZI WA TBC...

Mfanyakazi wa Shirika la Utangazaji  Tanzania (TBC1), Ramadhan Gize ameuawa kwa kupigwa risasi na  majambazi usiku wa kuamkia jana jijini Dar es Salaam.
Gize, ambaye alikuwa dereva wa shirika hilo, aliuawa usiku katika eneo la Ubungo Maziwa wakati akiwa  kazini, akienda kuchukua wafanyakazi kuwapeleka kazini kwa zamu ya usiku.
Kulingana na taarifa kutoka TBC, alipigwa risasi akiwa ndani ya gari karibu na duka ambalo majambazi hao walikwenda kupora. Ilielezwa ilikuwa kabla ya saa 6 usiku.
Sanjari na dereva huyo, mtu mwingine, Mwarami Rajabu aliyekuwa jirani na duka hilo,  alijeruhiwa kwa kupigwa risasi na majambazi hao.
Gize ametumikia TBC kwa miaka saba tangu 2007. Msiba uko maeneo ya Ubungo Kibangu, wilayani Kinondoni kwa babake, Ismail  Gize.
Mwili wake utaagwa leo katika Hospitali ya Mwananyamala kabla ya kusafirishwa kwenda Magole mkoani Morogoro kwa maziko. Alizaliwa Januari mosi 1968 na ameacha watoto watatu.
Taarifa ya habari ya TBC1  iliyomkariri Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura,  ilisema hadi jana hakuna aliyekuwa amekamatwa kuhusika na mauaji hayo. Hata hivyo, kamanda alisema wanaendesha msako kubaini wahusika.

No comments: