Monday, November 4, 2013

DK. SENGONDO MVUNGI ACHARANGWA MAPANGA NA MAJAMBAZI, YUKO HOI ICU...

Wauguzi wakimpeleka Dk Sengondo Mvungi kwenye Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU) jana.
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Mkuu wa Idara ya Katiba na Sheria wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Dk Sengondo Mvungi, amejeruhiwa vibaya na mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi ambao walivamia nyumbani kwake usiku wa manane.

Kwa sasa hali ya kiongozi huyo, ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Bagamoyo, ni mbaya na amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi katika Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI).
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema Dk Mvungi alipatwa na mkasa huo baada ya watu wasiojulikana kuvamia nyumbani kwake na kumcharanga mapanga maeneo mbalimbali mwilini, ikiwemo kichwani hadi akapoteza fahamu.
Alisema Dk Mvungi alivamiwa usiku wa kuamkia jana saa nane usiku ambapo baada ya kuvamiwa na kujeruhiwa na watu hao, alikimbizwa hospitali ya Tumbi, Kibaha ambako alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Alifikishwa Muhimbili saa 11 alfajiri na kupelekwa eneo la mapokezi ya dharura na baadaye alihamishiwa wodi ya Taasisi ya Mifupa (Moi) kwa ajili ya kuanza matibabu.
“Tulimleta hapa Moi, lakini kuna vipimo imeshindikana kupimwa hapa hivyo, tumempeleka Aga Khan kumpima na kumrejesha na sasa amepumzishwa ICU na anatakiwa asisumbuliwe kwa saa 72,” alisema Mbatia.
Mbatia alisema wakati Dk Mvungi aliporejeshwa Muhimbili, hali yake ilikuwa mbaya kwani alishindwa hata kuwatambua baadhi ya watu na hivyo, kutakiwa kupumzika bila kubughudhiwa kwa saa hizo 72.
Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uhusiano wa Umma wa NCCR-Mageuzi, Moses Machali, alikiri kuwa na taarifa za tukio hilo ambazo alizipata kutoka kwa ndugu wa Dk Mvungi, ambao walimpigia simu juzi usiku.
Alisema kwa mujibu wa ndugu wa kiongozi huyo, watu hao wanaodhaniwa kuwa majambazi walivunja mlango wa nyumba ya Dk Mvungi iliyopo Kibamba na kuanza kumshambulia kwa mapanga na kumjeruhi vibaya kichwani.
“Mpaka sasa hatujapata taarifa za wizi ila ninachofahamu ni kwamba walivunja mlango na kutaka fedha, na baada ya hapo walimshambulia Dk Mvungi na mjukuu wake,” alisisitiza Machali.
Mwandishi aliwasiliana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Saalam, Suleiman Kova, ambaye alisema atafutwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura azungumzie vizuri tukio hilo.
Hata hivyo jitihada za kumpigia simu Kamanda Wambura, hazikuzaa matunda kwa kuwa simu yake ambayo mwandishi alipatiwa na Kamanda Kova, ilikuwa imezimwa.

No comments: