Monday, November 4, 2013

BARAZA LA MAWAZIRI SASA KUJADILI MGOGORO WA AFRIKA MASHARIKI...

Dk Richard Sezibera.
Baada ya kuwa kimya juu ya mgogoro wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC), hatimaye Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dk Richard Sezibera, ameibuka na kusema kuwa mgogoro miongoni mwa nchi wanachama utajadiliwa kwa kina katika kikao kijacho cha Baraza la Mawaziri.

Kikao hicho cha mawaziri kwa mujibu wa Dk Sezibera, kitafanyika Novemba 28 mwaka huu. Kikao hicho ndicho kikao cha juu ambacho kinatoa mapendekezo mbalimbali yanayoenda kujadiliwa kwenye vikao vya wakuu wa nchi wanachama.
Dk Sezibera ambaye ni raia wa Rwanda ndiye anayeongoza Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye makao yake makuu mjini Arusha na alikuwa hajasema lolote tangu kuanza utaratibu wa nchi tatu kukutana bila kushirikisha Tanzania na Burundi na wala haijajibu malalamiko  ya Serikali ya Tanzania.
Katika  taarifa yake, Katibu Mkuu huyo alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa nchi za Burundi na Tanzania kuhusu wasiwasi  wa  vikao kadhaa vilivyofanywa na viongozi wakuu wa nchi za Kenya, Rwanda na Uganda bila kushirikisha wanachama wenzao.
Kwa muda sasa muungano huo haramu wa nchi tatu umekuwa unaripotiwa kwa kina na vyombo vya habari kuhusu kutengwa kwa nchi hizo mbili, lakini sekretarieti hiyo iliendelea kuwa kimya. Tanzania ilitoa tamko la wazi kuwa nchi hizo zimekiuka makubaliano yaliyoko kwenye mkataba wa jumuiya hiyo.
"Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ameshauriana na nchi tano wanachama kuhusu suala hilo," alisema Dk Sezibera na kuongeza kuwa katika mkutano wa 19 wa Baraza la Mawaziri wa kisekta, alibadilisha mawazo na mawaziri na wote  walionesha nia ya kuendelea kujenga jumuiya hiyo, ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto zilizojitokeza.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu huyo amewaomba  wananchi wa Afrika Mashariki  wasishtushwe na changamoto zinazojitokeza; kwani zinashughulikiwa na zitajadiliwa kwa kina katika mkutano wa mawaziri ambao utafanyika Novemba 28 na utatoa mapendekezo juu ya kilichojiri kwenye mkutano huo.
Alisema nchi wanachama zimedhamiria kuanza utekelezaji wa itifaki za soko la pamoja na ushuru wa forodha, ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa miundombinu, kuondoa vikwazo kwenye  usafirishaji wa mizigo ya  biashara, huduma na watu.
Rais  Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda na Uhuru Kenyatta wa Kenya juzi walikutana tena mjini Kigali, Rwanda  pamoja na mambo mengine, walitarajia kusaini makubaliano ya kuanzisha kituo kimoja cha kukusanya ushuru kinachotarajia kurahisisha uchukuzi wa bidhaa kutoka Mombasa nchini Kenya, Uganda hadi Rwanda. Katika mkutano huo Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini alialikwa kama mshirika.
Mkutano huo ulifanyika baada ya ule uliofanyika mjini Kampala, Uganda, Juni mwaka huu na mwingine uliofanyika Mombasa, Agosti, ambako viongozi hao watatu walipendekeza kupanuliwa kwa Bandari ya Mombasa, ili kuwezesha uharaka wa bidhaa kupitishwa katika kuhudumia Kanda nzima.
Hivi karibuni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alitangaza kuwa Tanzania itatoa ‘talaka’ kwa nchi za Rwanda, Kenya na Uganda ambazo zimeamua kuanzisha Jumuiya ya hiari nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Sitta alisema kutokana na nchi hizo kuonekana kuitenga Tanzania na Burundi ambazo ni wanachama wa jumuiya hiyo, wameshaanza mazungumzo ya kushirikiana kiuchumi, kisiasa na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo (DRC).
“Hawa wenzetu wanafanya utoto wa kutuzunguka, sisi tunatumia hekima za mzee Mwinyi aliyesema ‘mwongo, mwongoze’. Kama wao wana hila zozote juu yetu, siku si nyingi tutazibaini, kama ni ndoa kwenye jumuiya basi sisi ndio tutakuwa tumeoa…hivyo tutatoa talaka wakati wowote,” alisema Sitta baada ya kutakiwa kutoa ufafanuzi na Wabunge.

No comments: