Sunday, October 20, 2013

WATAKA TRAFIKI WA KUVUSHA WALEVI BARABARANI DODOMA...

Moja ya mitaa ya Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi amekataa ombi la wakazi wa eneo la Chaduru katika Manispaa ya Dodoma kutaka kuwepo kwa Askari wa Usalama Barabarani  kwa ajili ya kuvusha walevi ambao wamekuwa wakigongwa kwa wingi katika eneo hilo.

Dk Nchimbi alikataa ombi hilo juzi wakati alipotembelea na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo ikiwa  siku ya kilele cha Siku ya Usalama Barabarani.
Mmoja wa wakazi hao, Athumani Abdallah alisema ajali nyingi zinazotokea katika eneo hilo kwa kuwa lina vilabu vingi vya pombe za kienyeji jambo ambalo linasababisha walevi kugongwa mara kwa mara wanapokuwa wakivuka barabara.
"Tunaomba Serikali kuweka askari ili kuvusha walevi katika eneo hili ili wasiendelee kupoteza maisha kutokana na kugongwa na magari," alisema.
Kauli hiyo ambayo ilizusha kicheko ilipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye alisema kuwa, Serikali  haiwezi kufanya kitu kama hicho na hakuna serikali yoyote duniani yenye utaratibu wa kuvusha walevi. Alisisitiza kinachotakiwa ni walevi kuwa makini wanapovuka barabara.
"Muwe mnakunywa kwa kiasi si kwa kupitiliza mtu analewa hadi anakosa kumbukumbu na kufahamu kuwa hii ni barabara na anatakiwa kupita kwa uangalifu," alisema.
Aliwataka wananchi hao kuheshimu alama za Usalama Barabarani na hata kulinda alama hizo badala ya kuzitoa hali inayofanya magari kukosa ishara ya kutambua kama kuna alama au michoro katika eneo hilo.
Wakati huo huo, jumla ya watu 727 wamepoteza maisha mkoani hapa kutokana na ajali za barabarani katika kipindi cha mwaka 2010 hadi Septemba mwaka huu.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Dodoma, Peter Sima alisema watu hao walipoteza maisha katika ajali 585 zilizotokea zikahusisha vifo hivyo katika maeneo mbalimbali mkoani Dodoma.
Alisema mbali na ajali hizo za barabarani pia jumla ya ajali 784 zilizotokea katika kipindi hicho zilisababisha watu 1919 kujeruhiwa.
Pia  alisema katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu ajali za barabarani 20 zilipungua kutoka ajali 313  kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka 2012 hadi ajali 293 katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2013.
Alisema katika kipindi hicho pia ajali zilizohusisha pikipiki zilipungua  na kutoka ajali 93 hadi ajali nane sawa na asilimia 8.6 kwa kipindi cha Januari hadi Septemba 2013.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2010 hadi Septemba mwaka huu vifo vilivyotokana na ajali za pikipiki vilikuwa 163 kati ya ajali 130 zilizohusisha vifo.
Alisema asilimia 78 ya ajali zinazotokea mkoani Dodoma zinasababishwa na makosa ya kibinadamu huku mwendo kasi na ulevi vikichangia kwa kiasi kikubwa.

No comments: