Monday, October 14, 2013

WANANCHI WAMPOPOA MAWE MKUU WA WILAYA YA MVOMERO...

DC Anthony Mtaka.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka, jana alijikuta katika mazingira hatari baada ya kupopolewa mawe wakati akijaribu kushawishi wananchi wafungue barabara ya Turiani  Morogoro, waliyoifunga kuanzia alfajiri.

Wananchi hao zaidi ya 400 wanaolima katika bonde la Mgongola, wilayani Mvomero, walifunga barabara hiyo kwa siku nzima na kukwamisha huduma za usafiri wa magari ya abiria na mizigo.
Hatua hiyo ya wananchi ililenga kushinikiza uongozi wa wilaya na mkoa, kutatua mgogoro kati yao na wafugaji uliodumu muda mrefu. Kutokana na hatua hiyo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ikiongozwa na  Mtaka, ililazimika kufika eneo hilo kutafuta suluhu.
Baada ya kufika eneo la tukio, alishuka katika gari lake ambalo lilipaki mbali na eneo hilo na kuwafuata wakulima katika mashamba yao kuzungumza nao ili wafikie muafaka.
Alipofika katika mashamba yao, aliwakuwa wakulima hao na kuzungumza nao ambapo alikiri kuwa mgogoro kati ya wakulima na wafugaji juu ya nani anastahili kumiliki Bonde la Mgongola, ni wa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, mbali na mgogoro huo kuwa wa muda mrefu, pia kuna kesi imefunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na sasa kinachosubiriwa ni uamuzi wa Mahakama.
Kutokana na kesi hiyo, Mtaka alisema uongozi wa wilaya umeona ni vyema wakulima waendelee na shughuli za kilimo, wakati wakisubiri uamuzi utakaotolewa na Mahakama.
Wakati Mtaka akiendelea kuwashawishi wananchi hao kufungua barabara hiyo, wakulima haohao walikuwa wakipiga kelele wakisema wanamtaka Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera, aje kwa kuwa yeye kwa muda mrefu ameshindwa kupata suluhu ya mgogoro husika.
Wakizungumza kwa jazba mbele ya Mtaka, wakulima hao walikataa katakata kumsikiliza licha ya Mkuu huyo wa Wilaya kuendelea kuwasihi wamsikilize bila mafanikio.
Katika hali ambayo haikutarajiwa, walianza kurusha
mawe upande alikosimama Mtaka na viongozi wenzake wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, huku wakiwafuata wakiwa wameshika fimbo.
Kutokana na hali hiyo, askari Polisi walilazimika kufyatua mabomu ya machozi na risasi baridi hewani, ili kutawanya wakulima hao, na wakati huo huo kumtorosha Mtaka na viongozi wenzake, ambapo Mkuu huyo wa Wilaya aliingizwa katika gari la Polisi kwa kuwa gari lake lilikuwa mbali.
Hata hivyo jitihada za Polisi kutawanya wakulima hao  hazikufua dafu kutokana na kukabiliwa na  mashambulizi ya mawe na fimbo hali iliyosababisha gari lenye namba SM 4503, linalotumiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Wallace Karia, na gari la Mkuu wa Wilaya, kuvunjwa vioo.
Licha ya kuharibu magari hayo, pia katika vurugu hizo, wakulima hao walimjeruhi kwa jiwe Askari PC Nelson, ambaye alipigwa na kuumizwa sehemu ya mdomoni na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.
Hadi kufikia saa 12 jioni ya jana wakulima hao walikuwa bado hawajaondoka sehemu ya makutano ya barabara kuu ya Turiani Morogoro katika kijiji cha Dihombo na Mkindo.
Kutokana na kuzidiwa, askari Polisi nao walilazimika kuondoka kwenda kujipanga upya, ili kujerejea kufungua barabara hiyo na kuweka udhibiti mkali kwa kuongeza askari zaidi.
Mtaka alipozungumza na gazeti hili, alilaani kitendo cha wakulima hao kufunga barabara ambayo inatumiwa na wasafiri  wakiwemo wagonjwa, wajawazito na wananchi wa kawaida pamoja na kurushia mawe vyombo vya ulinzi na usalama.
Alisema vyombo hivyo vya usalama vilikuwepo hapo kuangalia usalama na tatizo lao lilikuwa linazungumzika.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye hakupenda jina lake litajwe, alidai barabara hiyo ilizibwa kuanzia saa nane usiku wa kuamkia jana.
Alidai baada ya wananchi kuweka vizuri barabarani kuanzia usiku wa manane, jana asubuhi askari Polisi kutoka Turiani walifika eneo hilo na kuanza kurusha mabomu ya machozi jambo ambalo lilifanya wananchi hao kujihami kwa kurusha mawe.
Shuhuda huyo alidai baadaye magari ya Polisi yaliongezeka kwa kuongeza idadi ya askari kutoka Turiani na Dakawa, lakini wananchi walizidi kujihami na mawe ambapo askari Polisi walizidiwa nguvu tena.

No comments: