![]() |
| Kero kama hizi kwa wasafiri wa Treni ya Reli ya Kati zinatarajiwa kuisha mwakani. |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka, alisema Dar es Salaam jana kuwa Serikali tayari imeshalipia asilimia 50 ya ununuzi wa vichwa 13 vya reli hiyo.
“Mabehewa 274 yameshalipiwa hivyo tutegemee mabadiliko makubwa katika Reli ya Kati na mabadiliko haya yataonekana kuanzia mwaka kesho,” alisema.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (MMS), mkutano wa saba uliowahusisha wadau mbalimbali wa maendeleo na sekta ya usafirishaji, Dk Mwinjaka alisisitiza kuwa ifikapo mwaka kesho, usafiri wa Reli ya Kati utakuwa wa uhakika.
Alisema tayari vichwa vinane vinakarabatiwa na vingine 13 vimeshalipiwa na vitapatikana mwakani kati ya Julai na Agosti.
Aidha, alisema kuwa katika Reli ya Kati, madaraja 28 yanatakiwa kukarabatiwa kwa kuwa mengi yamechakaa, na yalijengwa enzi za ukoloni ambapo mpaka sasa wameshakarabati madaraja matatu.
Kwa upande wa Bandari, wanatarajia kufanya matengenezo katika magati na kupunguza vituo vya magari katika barabara kuu kutoka 15 hadi kufikia vituo vitatu.
Akifungua mkutano huo, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alisema kutokana na mizigo mingi mikubwa kupitishwa katika barabara, wameweka nguvu katika kuboresha reli ili kupunguza mizigo katika barabara.
Alisema pamoja na kupunguza vizuizi barabarani, wataweka mizani ya kisasa itakayojengwa vigwaza kwa ajili ya kupima mizigo kitaalamu zaidi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wakala wa ForodhaTanzania (TAFFA), Solomon Kasa, aliiomba Serikali kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, kuongeza nguvu zaidi katika kuboresha usafiri wa reli kwa kuwa kwa sasa barabara zimeelemewa na mizigo.

No comments:
Post a Comment