![]() |
| Shekhe Ponda Issa Ponda. |
Upande wa mashitaka katika kesi ya uchochezi inayomkabili Katibu wa Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Shekhe Ponda Issa Ponda, umedai kuwa upelelezi umekamilika.
Kutokana na hatua hiyo, Wakili wa Serikali Bernald Kongola, alipendekeza jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, Richard Kabate, kuwa kesi hiyo ianze kusikilizwa mahakamani hapo kuanzia Oktoba 10, mwaka huu.
Hata hivyo mawakili watatu wanamwakilisha Shekhe Ponda, Juma Nassoro, Ignas Punge na Batholomeo Tarimo hawakuwepo mahakamani.
Badala yake Wakili Yahaya Njama aliyekuwa akimtetea Shekhe Ponda katika kesi ya awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Jijini Dar es Salaam, alifika kuomba udhuru wa Wakili Nassoro, ambaye ilidaiwa yupo nchini India kwa matibabu ya macho.
Alidai kuwa Wakili Nasoro aliondoka nchini Septemba 25, mwaka huu na anatarajiwa kurejea Oktoba 25, mwaka huu baada ya afya yake kutengemaa.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Kongola alisisitiza pendekezo lake la kesi hiyo ianze kusikilizwa mahakamani hapo kuanzia Oktoba 10, mwaka huu, kwa maelezo kuwa Shekhe Ponda anatetewa na mawakili watatu.
Kutokana na hoja hiyo, Hakimu Kabate alitoa barua iliyoandikwa na Wakili Tarimo na kuisoma mahakamani hapo ambayo aliomba udhuru wa kutofika mahakamani kwa siku hiyo.
Naye Njama, alidai mahakamani hapo kuwa, yeye
hatambui uwepo wa mawakili hao wawili zaidi ya Nasoro ambaye alimwagiza amwakilishe jana katika kesi hiyo.
Hata hivyo, Hakimu Kabate alisema yeye anawatambua mawakili hao kwa kuwa wamekuwa wakishiriki mwenendo wa kesi hiyo na tayari kuna kumbukumbu za maandishi mahakamani hapo. Alisema ikiwa wamejitoa walitakiwa kutoa taarifa kwa maandishi.
Kutokana na hatua hiyo wakili Yahya alioomba Mahakama iwape muda na kwamba watalishughulikia hilo suala la kupeleka taarifa sahihi Mahakamani hapo.
Ponda katika kesi hiyo anadaiwa kufanya makosa ya uchochezi, ambapo la kwanza la uchochezi analoshitakiwa nalo ni madai ya kusema: "Ndugu Waislamu msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata (Baraza la Waislamu Tanzania) ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali.
"Kama watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya msikiti yenu, muwapige sana."
Shekhe Ponda anadaiwa kwa kauli aliumiza imani za watu wengine, na ni kinyume cha hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, iliyotolewa na Hakimu Victoria Nongwa Mei 9, mwaka huu ambayo ilimtaka ndani ya mwaka mzima kuhubiri amani.
Katika kosa la pili Shekhe anadaiwa kuwa Agosti 10 mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, mshitakiwa alitoa maneno yenye nia ya kuumiza imani nyingine za dini.
Shekhe Ponda katika kosa hilo anadaiwa kusema: "Serikali ilipeleka Jeshi Mtwara kushughulikia vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka, na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu.
"Lakini Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji, baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo."
Maneno hayo hayo anayodaiwa kusema Shekhe Ponda, yanadaiwa kuumiza imani za watu wengine na ni kinyume cha kifungu cha sheria 129 cha 2002.
Katika kosa tatu, Shekhe Ponda anadaiwa kwa maneno hayo ya "Serikali kupeleka jeshi Mtwara" alishawishi Waislamu kujumuika kinyume na sheria.

No comments:
Post a Comment