![]() |
| Profesa Eustella Bhalalusesa. |
Akizungumza na mwandishi wiki iliyopita, Kamishna wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa, alisema wanataka kazi anazofanya mwanafunzi shuleni, zitumike katika kumpatia alama ya ufaulu katika mtihani wa mwisho.
Katika mfumo huo mpya, kwa mujibu wa Profesa Bhalalusesa, wanafunzi wakati wanakwenda kufanya mtihani, watakuwa tayari wanajua alama za mchango wa kazi shuleni, na kuwa na hakika ya anachokwenda kufanya katika mtihani.
“Miaka ya nyuma, hakuna mwanafunzi aliyekuwa akijua alama aliyoipata imepangwa vipi, tunaona kuna haja ya kila mwanafunzi akiingia kwenye mtihani wake wa mwisho awe anajua anakwenda kutafuta nini,” alisema.
Kwa maana hiyo, kama mtihani una alama 100, mwanafunzi anaweza kutakiwa kutafuta alama 50 kupitia kazi za shule na alama 50 katika mtihani wa mwisho.
Mfumo huo unaotumika vyuo vikuu nchini ukianza, kabla ya kuanza mtihani wa mwisho, mwanafunzi atakuwa akijua kati ya hizo alama 50, amepata ngapi kabla ya kuingia katika mtihani wa mwisho.
“Hatutaki kuona mwanafunzi hanufaiki na kile alichokivuna akiwa shule. Mfano mfumo wa sasa mwanafunzi aliyepata alama F ni aliyepata alama kati ya 0-34.
“Lakini hapo kuna wanafunzi ambao wamezidiana kwa mfano aliyepata alama 20, hawezi kuwa sawa na aliyepata 0 ingawa wote wanawekwa kundi la F,” alifafanua Profesa Bhalalusesa.
Tayari Serikali imetuma dokezo, ambalo lipo katika tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa wadau wa elimu ili kupata maoni yao kabla ya kuanzisha mfumo huo.
Dodoso hilo limeeleza kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, imeelekeza kwamba katika kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi wa elimu ya sekondari, Alama za Tathmini Endelevu ya Mwanafunzi zitachangia asilimia hamsini na mtihani wa mwisho utachangia asilimia hamsini pia.
“Hata hivyo, kumekuwa na mitizamo, maoni na mapendekezo tofauti katika muundo na matumizi ya Alama za Tathmini Endelevu ya Mwanafunzi. Mfumo huu hata hivyo hautumiki kwa wanafunzi wa kujitegemea,” lilieleza dokezo hilo.

No comments:
Post a Comment