Thursday, October 31, 2013

UJENZI WA DARAJA KUBWA LA MALAGARASI WAKAMILIKA...

Lori likipita juu ya Daraja la Malagarasi.
Ujenzi wa Daraja la Malagarasi lililopo mkoani Kigoma, maarufu kama Daraja la Kikwete, umekamilika rasmi na tayari magari yameanza kulitumia.

Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, akiwa ziarani mkoani humo, alitembelea eneo hilo na kujionea magari yakipita katika daraja hilo.
Akizungumza baada ya kumaliza ziara hiyo, waziri huyo  alisema ameridhishwa na utendaji wa mkandarasi ambaye ni  M/S Hanil Engineering and Construction Company Limited kutoka Korea Kusini.
Alisema mkandarasi huyo, amekamilisha ujenzi wa daraja hilo sehemu ya kwanza kwa mujibu wa mkataba na kwa viwango vya hali ya juu.
"Nimeridhishwa na utendaji wa mkandarasi huyu na hasa kwa jinsi alivyoweza kumaliza sehemu hii ya kwanza kwa muda mzuri na viwango vya hali ya juu," alisisitiza Magufuli.
Kwa muda mrefu usafiri katika eneo hilo, ulikuwa ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya Mkoa ya Kigoma, hasa nyakati za mvua, kutokana na kukosekana kwa daraja la uhakika.
Baada ya kukamilika kwa daraja hilo, sasa kuna ongezeko kubwa la magari kati ya Manyoni-Itingi -Tabora hadi Kigoma kupitia katika Daraja hilo la Kikwete.
Awali ililazimu magari hayo kupitia barabara ya Manyoni -Singida - Nzega - Kahama - Nyakanazi Ð Kibondo - Kasulu hadi Kigoma.
Kampuni ya M/S Hanil iliingia mkataba na kuanza ujenzi wa daraja hilo Desemba mwaka 2010. Ilitakiwa kukamilisha kazi hiyo ifikapo Desemba, mwaka huu.
Mradi huo unajumuisha ujenzi wa madaraja matatu, yenye urefu wa mita 275  pamoja na barabara ya lami, yenye urefu wa kilometa 48 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 64, ambazo ni sawa na Sh bilioni 90 zilizotolewa na Benki ya Exim ya Korea Kusini kwa asilimia 90. Kiasi kilichobaki ni fedha za ndani.
Akizungumzia mradi huo, Mhandisi Yu Sing kutoka kampuni ya Hanil Engineering, alisema mradi huo umegawanywa katika sehemu  mbili.
Sehemu ya kwanza iliyokamilika  ni ya ujenzi wa madaraja matatu yenye urefu wa meta 25, meta 200 na meta 50 na kilometa 11 za lami. Sehemu ya pili ni ujenzi wa kilometa 37 za lami, ambazo ndizo zinazoendelea kukamilishwa kwa sasa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, kwa niaba ya wananchi wa Kigoma, kwa kutimiza ahadi ambayo imekuwa ikisuburiwa muda mrefu.
"Kukamilika kwa mradi huu na mingine inayoendelea kujengwa katika barabara ya Kigoma kuelekea Tabora hadi Manyoni mkoani Singida, ni ufumbuzi mkubwa wa matatizo yaliyokuwa yakikwamisha maendeleo katika ukanda huu wa Magharibi," alisisitiza Machibya.

No comments: