| Abiria katika Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo, Dar es Salaam. |
Baadhi ya mabasi yanayofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa mbalimbali nchini, jana yaligoma kusafirisha abiria kwa saa kadhaa.
Yalifanya hivyo kushinikiza Serikali isitekeleze Sheria ya Barabara inayotaka mzigo ukizidi tani 56, mmiliki atozwe faini.
Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), kinataka Serikali isitoze faini magari yenye uzito usiozidi asilimia tano, juu ya tani 56 zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.
Kutokana na msimamo wa Serikali uliotangazwa mwanzoni mwa mwezi huu kuwa atakayezidisha uzito atatozwa faini, Taboa kiliamua kusitisha usafiri kwa abiria, wakiwemo wagonjwa na waliokuwa wakisafiri kwa ajili ya shughuli mbalimbali, ikiwemo misiba.
Abiria waliokuwa katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo (UBT), walijikuta wakikumbana na adha ya kukosa usafiri iliyodumu kwa zaidi ya saa tatu kuanzia Saa 12.00 asubuhi hadi saa 3.21.
Wakati mgomo huo ukiendelea, baadhi ya mabasi ya Kampuni za Dar Express, Taqwa, Metro East African, Tawaqal, Tahmeed, Raha Leo, Smarts, Ratco Express na Modern, yaliendelea na safari zao.
Mabasi hayo yaliondoka na abiria kituoni hapo, huku wakiacha gumzo kwa baadhi ya viongozi wa Taboa, waliokuwa wakidai kuwa wamesalitiwa.
Mabasi hayo yakiongozwa na Metro East African No. KBV 664E, lililokuwa likielekea Kampala nchini Uganda, yalianza kutoka kituoni hapo Saa 1.38 kwa kutumia geti la kuingilia. Polisi ilikuwa imeimarisha ulinzi dhidi ya baadhi ya watu, waliokuwa wakitishia kuzuia mabasi kutoka getini.
Wakati mabasi hayo yakiendelea na mgomo, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Barabara kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra), Gilliad Ngewe alikuwa katika kikao cha dharura na Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Kanda ya Mashariki, Conrad Shiyo na viongozi wengine wa mamlaka hiyo.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama wa Barabarani, Mohammed Mpinga na uongozi wa Taboa, wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Severine Ngaro.
Baada ya kikao hicho saa 3.21 za asubuhi, mabasi yalianza kutoka mfululizo kwa kutumia milango yote miwili.
Viongozi hao kwa pamoja walikubaliana mabasi yote kwa jana, yasafiri bila kupima katika mizani, ili kuwaondolea usumbufu zaidi abiria kwa jana wakati suala hilo likitafutiwa ufumbuzi.
Akizungumzia suala hilo, Ngewe alisema wamiliki wa mabasi walistahili kuchukuliwa hatua pale pale kwa kuwaandikia faini, lakini waliamua kutumia busara kwa lengo la kunusuru tatizo lililokuwepo.
“Kwa kitendo hiki Taboa wamekiuka masharti ya leseni, wao wana mkataba na abiria, hawakupaswa kugoma kwa kuwa tayari walishawakatia tiketi abiria kwa ajili ya safari.
“Ili kuwaondolea usumbufu walioupata abiria kwa zaidi ya saa tatu, tuliwasiliana na Tanroads (Wakala wa Barabara) na Waziri John Magufuli, ambaye ametoa idhini kwa mabasi kusafiri bila kupima katika mizani kwa leo tu,” alisema Ngewe.
Ngaro alipongeza uamuzi wa kuruhusu mabasi kusafiri bila kupima kwa jana. Alidai kuwa mgomo huo ni endelevu hadi madai yao yatakapofanyiwa kazi.
“Tunawaomba abiria na wananchi wanaotarajia kusafiri kesho (leo), wasikate tiketi kwa kuwa hatutarajii kuendelea kutoa huduma hadi pale tutakapowatangazia, vinginevyo hatutahusika na usumbufu watakaoupata.
“Pamoja na Dar es Salaam mgomo huu pia unafanyika Arusha, Mbeya na Mwanza… kikubwa hapa ni ufafanuzi wa sheria iliyopo ambayo imepelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali… tusubiri ni namna gani ataifafanua,” alisema Ngaro.
Akizungumza na mwandishi kwa simu jana, Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Haki za Abiria (CHAKUA), Hassan Mchanjama alisema wapo katika mchakato wa kujua ni abiria wangapi wameathirika na mgomo huo, wakati wakiandaa mashitaka kwa ajili ya kuyapeleka kwa mamlaka zinazohusika.
Alisema imekuwa ni kawaida kwa wamiliki wa mabasi, kuwatumia abiria kuwa silaha ya kutekeleza matakwa yao kwa kufanya migomo. Aliongeza kuwa kwa sasa suala hilo wameamua kulivalia njuga, ili kulinda haki za abiria.
Taarifa hizo wanazozikusanya, zitakuwa ushahidi wa malalamiko ya abiria mbalimbali wakiwemo waliokuwa wakisafiri kwenda katika misiba, wagonjwa, wafanyabiashara na wengine.
Mamia ya abiria wakiwemo wanawake watoto na wazee, walionekana kuwa katika simanzi iliyosababishwa na adha hiyo huku wengi wao walilaumu mamlaka zote zilizohusika katika tatizo hilo.
“Hatuelewi kwa nini tumekuwa tukifanyiwa ukatili huu usio na tija kila wakati wakati viongozi wote wapo na wanauwezo wa kukaa meza moja kutafuta ufumbuzi.
“Kwao inaweza kuwa faida, lakini kwetu hapa ni shida tupu,” alisema Abdalla Chuji aliyekuwa akisafiri na basi la Kiruto Express kwenda Kondoa.
Mama wa watoto wadogo mapacha, Margaret Maaghina aliyekuwa akisafiri na basi la Taqwa kwenda Bukoba, huku akitokwa na machozi, alisema alikuwa akiwahi maziko ya ndugu yake.
“Mazishi yamepangwa kufanyika kesho saa 7 mchana, kwa kawaida kama tungewahi kuondoka, hadi kesho saa sita mchana tungekuwa tumefika, kwa hali hii sijui tutafika muda gani,” alisema Margaret.
Mkoani Arusha mabasi yanayofanya safari zake kwenda mikoa ya Tanga na Dar es Salaam, yaligoma kuondoka Kituo Kikuu cha Mabasi kwa zaidi ya saa tatu na kusababisha abiria kushindwa kujua hatma yao.
“Tutaondoka hapa, lakini hatujui tutawapeleka wapi abiria na safari yetu itakapokwamia ni hapo hapo, lakini huku ni kutesa abiria, bora tungeacha kuwachukua hapa kituoni, mpaka mgomo umalizike,” alisema mmoja wa madereva hao, Swalehe Amuri.
Madereva hao waliomba Serikali kufuata utaratibu kama wa nchi jirani ya Kenya na Uganda, ambao walidai hawana sheria hiyo ya mizani.
No comments:
Post a Comment