Thursday, October 24, 2013

MWILI WA KAMANDA JAMES KOMBE KUAGWA KESHO...

Marehemu Kamanda James Kombe.
Mwili wa aliyekuwa Kamanda mstaafu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) James Kombe, utaagwa kesho katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),  Usharika wa Msasani jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa kamati ya mazishi inayojumuisha familia ya marehemu na maofisa wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishina wa Polisi (DCP), Thobias Andengenye, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema  ndugu,  jamaa, marafiki maofisa wa Polisi, askari pamoja na viongozi mbalimbali, watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu na baadae  utasafirishwa kwenda Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya maziko.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, kutokana na kifo cha Kamanda Kombe.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha aliyepata kuwa Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani hapa nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) mstaafu James Kombe.
“Nilimfahamu Kombe, enzi za uhai wake, kama askari shupavu, mtiifu na mwaminifu aliyejituma vilivyo katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Kwa hakika sifa hizi ndizo zilizochangia kwa kiasi kikubwa kupandishwa cheo na kushika nyadhifa mbalimbali za juu hadi kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD); Mkuu wa Polisi wa Mkoa (RPC); Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), na hatimaye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, cheo alichokitumikia  hadi alipostaafu 2010,” alisema Rais Kikwete katika salamu hizo.
Alisema utumishi huo uliotukuka wa Kamanda Kombe ndani ya Jeshi la Polisi, ni wa kujivunia na wa kupigiwa mfano, ambao askari Polisi wengine hawana budi kuuiga ili Jeshi la Polisi liendelee kuaminiwa, kuheshimiwa na kupewa ushirikiano stahiki kutoka kwa wananchi.
“Kutokana na msiba huu, ninakutumia salamu za rambirambi wewe Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema kwa kumpoteza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi mstaafu Kombe.  Natambua fika kuwa licha ya kustaafu kwake, ushauri wake kwa jeshi letu la Polisi ulikuwa bado unahitajika sana,” alisema Rais Kikwete.
Amemuomba Kamanda Mwema kumfikishia salamu zake za rambirambi kwa familia ya marehemu Kombe na kuihakikishia familia hiyo kuwa yuko pamoja nao, katika kuomboleza kifo cha kiongozi ambaye ni mhimili madhubuti wa familia yao.
Alisema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi roho ya marehemu  Kombe. Pia ameiomba familia ya marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na ujasiri, wakati huu inapopitia machungu ya kuomboleza msiba wa mpendwa wao.
Kamanda Kombe alifariki dunia juzi wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.
Alizaliwa 1950 huko Mwika mkoani Kilimanjaro na alijiunga na Polisi Machi 15, mwaka 1970 baada ya kuhitimu elimu ya sekondari 1969 nchini Uganda.  Alipandishwa vyeo na kupewa madaraka mbalimbali.
Baadhi ya vyeo alivyopitia na miaka ya kupata vyeo hivyo katika mabano ni pamoja na Sajini wa Polisi (1973) Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (1977), Mkaguzi wa Polisi (1984), Mrakibu Msaidizi (1986), Mrakibu wa Polisi (1991), Mrakibu Mwandamizi (1995), Kamishna Msaidizi wa Polisi (1998) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (2002) hadi alipostaafu mwaka 2010.
Nafasi alizowahi kuzitumikia Polisi ni pamoja na kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) katika wilaya za Dodoma, Tarime, Serengeti na Arusha pamoja na Kuwa Mkuu wa Polisi wa Mkoa (RPC) katika mikoa ya Lindi, Arusha na Kigoma.
Pia aliwahi kuwa Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Tanzania na hadi anastaafu alikuwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania.

No comments: