![]() |
| Eneo la mizani ya barabarani Kibaha, mkoani Pwani. |
Msimamo wa Serikali kwa mujibu wa Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, ni kuzingatia sheria ambayo inataka magari hayo yasizidishe mzigo kupita kiwango cha juu kilichowekwa kisheria cha tani 56 kwa kila lori.
Wamiliki wa malori kupitia Chama cha Wamiliki wa Malori (TATOA), wanashinikiza Serikali irejee katika makubaliano ya mwaka 2006, ambapo waliruhusiwa kwa barua, kuendelea na safari bila kutozwa faini, kama mzigo utazidi tani 56, lakini si kwa zaidi ya asilimia tano.
Jana asubuhi, taarifa zilizotangazwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari na kusambaa, zilidai kuwa Dk Magufuli angezungumza katika ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), kuhusu mabadiliko ya msimamo huo.
Taarifa hizo zilisababisha ukumbi huo kujaa waandishi wakimtarajia Dk Magufuli, lakini wakaambulia kukutana na wamiliki wa malori.
Wakizungumza katika mkutano huo, wamiliki hao walidai hawajagoma na hawana sababu ya kugoma, badala yake wameegesha magari yao hadi hapo watakapopatiwa suluhu ya Sheria ya Barabara inayosababisha kuondolewa ruhusa ya kuzidisha mzigo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana Dar es Salaam, wamiliki hao walidai wao ni wafanyabiashara waliochukua mikopo katika mabenki mbalimbali na hawana sababu ya kugoma, bali wamepaki ili wasiharibu barabara.
Mmoja wa wamiliki hao, Davis Mosha alisema walipata barua inayohusu kuondolewa kiwango hicho cha ziada ya mizigo juu ya kiwango cha kisheria, lakini jambo lililowashangaza ni kukosa muda wa kujadiliana na mamlaka zilizohusika kutoa maamuzi hayo.
“Sisi hatujagoma, na wala hatutagoma, tumepaki ili tusiharibu barabara kwani tungepakia tungezidisha foleni barabarani…tunataka kufikisha kilio chetu kwa Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli ili suluhu ipatikane,” alisema Mosha na kuongeza wangeendelea kusafirisha mizigo na malori hayo, kungekuwa na msongamano mkubwa.
Alisema wao kama wasafirishaji ni wadau wakubwa katika kulinda miundombinu hiyo na hawako kwa ajili ya kubishana ila wanahitaji sheria kufuatwa.
Alisema kwa sasa mafuta hayaendi mikoani jambo ambalo linaweza kusababisha mgongano na kuiomba Serikali kutoa uamuzi haraka kuhusu sheria hiyo.
Kuhusu kwenda mahakamami kama hawakuridhika na uamuzi huo wa Serikali, alisema kuwa wao ni wastaarabu wanaotoa huduma katika jamii na hawakutaka kukurupuka kwenda mahakamani kudai haki yao ila bado wanaiheshimu Serikali yao.
Alisema haoni sababu ya kwenda mahakamani kwa kuwa bado wanasubiri Serikali itoe majibu kwani kuendelea kubishana wataonekana kutokuwa na nidhamu.
Mmiliki mwingine, Ibrahim Ismail kutoka Usangu Logistic, alisema wamepata usumbufu mkubwa na tatizo kubwa ni mizani kutokuwa na viwango vilivyo sawa.
Faisal Edha kutoka Overland Logistic, alisema asilimia hiyo haipo Tanzania peke yake, bali pia ipo katika nchi wanachama wa Jumuiya za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC).
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo alipoulizwa na gazeti hili kama Dk Magufuli alikuwa na mkutano wowote na waandishi wa habari leo, alisema hakukuwa na mkutano wa aina hiyo.
Badala yake alisema Wizara haijabadilisha msimamo na Dk Magufuli, ametoa pongezi kwa kampuni za usafirishaji ambazo zimekuwa zikiendelea na usafirishaji na hazijawahi kuzidisha uzito kwa miaka 10.
Alisema kampuni hizo zimekuwa mfano wa kuigwa kwa kuheshimu sheria na taratibu za usafirishaji hapa nchini kwa kujaza uzito unaotakiwa na chini ya hapo kiwango kilichowekwa na sheria.
“ Uchambuzi uliofanyika kwa kuangalia kipindi cha miaka 10, tumebaini kampuni ambazo hazina rekodi ya kuzidisha mizigo wakati wote magari yao yanapopimwa katika vituo vya mizani ya barabarani,” alisema na kuongeza kuwa kampuni za aina hiyo ni za kupongezwa kutokana na uzalendo na kuzingatia weledi katika uendeshaji wa shughuli zao za usafirishaji.
Magufuli alitaja kampuni hizo kuwa ni Dar Express, Cargo Star, Hood Bus, Coca-Cola, BM Coach, Bakhresa (AZAM Transport), Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Golden Coach, Kanji Lanji Bus, Taqwa, Consolidate Logistic, Lamada na BP ambayo sasa inaendeshwa na Puma.
Magufuli alisema Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ilitangaza upya nafasi za kazi katika mizani na kuwabadilisha wafanyakazi takribani 400, sawa na asilimia 85, hatua ambayo imedhibiti mianya ya kupitisha mizigo kinyume na taratibu na kukata mawasiliano kati ya wasafirishaji na watendaji hao.
Akizungumzia usahihi wa mizani, Kaimu Meneja Elimu na Mawasiliano wa Wakala wa Vipimo nchini, Irene John, alisema wamekuwa wakikagua mizani mara mbili kwa mwaka na kila zinapokaguliwa, hukutwa katika usahihi.
Hata hivyo alisema ipo tabia ya kuchezea mizani lakini kwa hizo za barabarani hawajawahi kukutana nayo lakini wakipata malalamiko, watafanya ukaguzi wa kushitukiza kubaini wanaofanya hivyo.

No comments:
Post a Comment