Wednesday, October 2, 2013

MAGAIDI WALIWATOROKA ASKARI WESTGATE MALL KUPITIA KWENYE MTARO...

Askari wa Kenya wakijipanga kupambana na magaidi hao katika jengo la Westgate Shopping Mall.
Inahofiwa kuwa baadhi ya magaidi wa kundi la al Shabaab, ambao walivamia maduka katika jengo la Westgate walitoroka kwa kutumia mtaro mkubwa wa maji machafu ulioko chini ya ardhi.

Habari zinaeleza kuwa al-Shabaab ambao waliua watu  68 baada ya kufanya uvamizi katika jengo hilo mjini Nairobi, walitumia njia za maji machafu ambazo ziliwawezesha kwenda kama nusu maili kutoka liliko jengo hilo, wakati askari walipokuwa wamelizunguka.
Baadhi ya picha zimeonesha kuwepo kwa mtaro huo wa maji machafu, ambao unaenda umbali mrefu hadi kutokea katika Mto Nairobi.
Ni katika mtaro huo wa maji machafu, ndiko  inasadikiwa kuwa magaidi hao walipitia na kutoroka baada ya kuwaua raia waliowateka katika maduka hayo.
"Walitoroka kama panya wa kwenye maji machafu, magaidi walipitia kwenye mtaro wa maji machafu ulio chini bila kujulikana.
"Tunashughulika na watu ambao wanajua wanachokifanya, operesheni iliyokuwa imepangwa na jeshi haikusaidia kuwanasa wote," taarifa zilieleza.
Mtaro unaopitisha maji machafu umejengwa kwa umbali kama wa maili mbili ndani ya Jiji la Nairobi, hali iliyowapa urahisi genge hilo la kigaidi kutoroka kabla ya majeshi ya Serikali kuwafikia.
Cha kushangaza mamlaka za kiusalama za Kenya, hazikubaini kuwa magaidi hao wangetumia mtaro huo   kutoroka hadi baada ya saa 12 baada ya utekaji huo kufanyika.
Taarifa za magaidi hao kutoroka kwa kutumia mtaro chini ya ardhi kama panya, zimekuja baada ya raia sita wa Uingereza kuuawa katika shambulizi lililofanyika Jumamosi.
Zaidi ya watu 150 wanahofiwa kupoteza maisha katika tukio hilo, kutokana na kuwepo taarifa za watu 62 waliokuwepo eneo la tukio ambao hawajulikani waliko.
Habari zinaeleza kuwa magaidi hao walipanga shambulizi hilo kwa muda mrefu, baada ya kusoma mfumo wa jengo ulivyo na kukodi duka walilotumia kuhifadhi silaha zao yakiwemo mabomu na bunduki.

No comments: