KESI ZOTE ZENYE ZAIDI YA MIAKA MITANO SASA KUPEWA KIPAUMBELE...

Fakih Jundu.
Jaji Kiongozi wa Tanzania, Fakih Jundu, ameagiza kesi zote  zilizokaa mahakamani kwa zaidi ya miaka mitano, kushughulikiwa haraka ili kuondoa mlundikano wa kesi.

Mbali na kuagiza kesi hizo kushughulikiwa, pia ameagiza  kesi zote mpya kushughulikiwa ndani ya miaka miwili,  ili kupunguza msongamano wa majalada ya kesi mahakamani.
Jaji Jundu alisema hayo jana wakati akiwaapisha wasajili wapya watano wa Mahakama, jijini Dar es Salaam.
Alisema wasajili hao watano, wameteuliwa ili kuongeza nguvu katika shughuli za kiutendaji za kimahakama.
"Tuko katika maboresho ya huduma zetu za kimahakama, kwa hiyo ni lazima tuongeze nguvu zaidi ili tuendane na dhamira yetu ya mashauri  yamalizike ndani ya miaka miwili.
"Bado hawa wasajili tutaendelea kuwaongeza hasa katika yale maeneo ambayo yana shughuli nyingi za kimahakama kwa sababu yapo maeneo hakuna mashauri mengi ya kusikilizwa kwa hiyo hii itasaidia kumaliza kwa haraka mashauri ya muda mrefu," alisema Jaji Jundu.
Wasajili walioapishwa ni Francis Kabwe ambaye amekuwa Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Lumuli Mbuya amekuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Dustan Ndunguru amekuwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, William Mutaki amekuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Elinaza Luvanda, ambaye amekuwa Msajili wa Wilaya ya Mahakama Kuu.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Kabwe alisema changamoto alizokuwa akikabiliana nazo wakati yuko Mahakama Kuu, zitakuwa ni zaidi, hivyo amejipanga vizuri kukabiliana nazo.
"Unapofanya kazi na ukajikuta umeongezewa majukumu ni wazi kuwa viongozi wako watatambua mchango wako, hivyo naamini kwa mimi wametambua mchango wangu. Kadri mambo yanavyozidi ndiyo changamoto nazo zinavyozidi hivyo nimejipanga vizuri kukabiliana nazo," alisema Kabwe.
Wakati huo huo, Jaji Mkuu wa Tanzania Mohammed Chande Othman amefanya mabadiliko katika mahakama tofauti, kwa kuwabadilisha mahakimu vituo vyao vya kazi.
Mahakimu hao waliobadilishwa vituo vyao vya kazi ni Joyce Minde, ambaye awali alikuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala sasa amekuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Singida, Mary Moyo ambaye alikuwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Mufindi sasa amekuwa Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Morogoro ; na Ally Nkasiwa aliyekuwa Hakimu wa Bagamoyo, kwa sasa amekuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Jiji.
Jaji Othman aliwakabidhi hati zao za uteuzi kwa ajili ya kuanza kazi katika vituo vyao vipya vya kazi.

No comments: