Tuesday, October 1, 2013

KESI YA SHEKHE PONDA KUENDELEA KUSIKILIZWA LEO...

Shekhe Ponda Issa Ponda.
Kesi inayomkabili Katibu wa Taasisi na Jumuiya ya Kiislamu Tanzania,  Shekhe Ponda Issa Ponda, inatarajia kuendelea kusikilizwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro.

Shekhe Ponda alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama hiyo Agosti 19, na leo itakuwa ni kwa mara ya tatu.
Alipofikishwa mahakamani Septemba 17, mwaka huu, mawakili wa Shekhe Ponda waliwasilisha ombi la kupata dhamana  ambalo hata hivyo Mahakama ilikataa kwa kukubali hoja za kupinga dhamana hiyo, zilizowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP).
Kesi hiyo ya Shekhe Ponda inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, Richard Kabate na  anakabiliwa na mashitaka matatu ya uchochezi anayodaiwa  kuyatenda Augosti 10, mwaka huu, eneo la Kiwanja cha Ndege katika Manispaa ya Morogoro.
Kosa la kwanza la uchochezi analoshitakiwa nalo ni madai ya kusema: “Ndugu Waislamu msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata (Baraza la Waislamu Tanzania) ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali.
“Kama  watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi  na usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya misikiti yenu, muwapige sana.”
Shekhe Ponda anadaiwa kwa kauli aliumiza imani za watu wengine, na ni kinyume cha hukumu ya Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, iliyotolewa na Hakimu Victoria Nongwa Mei 9,  mwaka huu ambayo ilimtaka ndani ya mwaka mzima kuhubiri amani.
Katika kosa la pili Shekhe anadaiwa kuwa Agosti 10 mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro,  mshitakiwa alitoa maneno yanye nia ya kuumiza imani nyingine za dini.
Shekhe Ponda katika kosa hilo anadaiwa kusema: "Serikali ilipeleka Jeshi Mtwara kushughulikia vurugu iliyotokana  na gesi kwa kuwaua, kuwabaka, na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu.
“Lakini Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji, baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo."
Maneno hayo hayo anayodaiwa kusema Shekhe Ponda, yanadaiwa kuumiza imani za watu wengine na ni kinyume cha kifungu cha sheria 129 cha 2002.
Katika kosa tatu, Shekhe Ponda anadaiwa kwa maneno hayo ya ‘Serikali kupeleka jeshi Mtwara’ alishawishi Waislamu kujumuika kinyume na sheria.

No comments: