Wednesday, October 30, 2013

HUKUMU YA BABU SEYA, PAPII KOCHA YAPITIWA LEO...

Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanawe Johnson Nguza 'Papii Kocha'.
Hukumu ya mwanamuziki maarufu nchini mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanawe Johnson Nguza 'Papii Kocha', inatarajiwa kufanyiwa mapitio leo na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa nchini.
Babu Seya na Papii Kocha wanaendelea kutumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kukutwa na hatia ya makosa ya kunajisi na kulawiti watoto wadogo.
Hukumu hiyo ilitolewa Februari 2010 na jopo la majaji wakiongozwa na Nathalia Kimaro. Majaji wengine ni Mbarouk Mbarouk na Salum Massati.
Watoto wawili wa Babu Seya, Nguza Mbangu na Francis Nguza waliachiwa baada ya kubainika kutokuwa na hatia kwa makosa ya kunajisi na kulawiti watoto.
Mapitio ya hukumu hiyo yanafanyika kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Mahakama ya Rufaa na majaji hao watatu waliotoa hukumu ya rufaa.
Babu Seya na Papii Kocha, Mbangu na Francis walihukumiwa kifungo cha maisha mwaka 2004 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Katika hukumu hiyo ya Juni 25, 2004, Hakimu Mkazi Addy Lyamuya aliwatia hatiani Babu Seya na wanawe watatu kwa makosa 23 ya unajisi na ulawiti na kuwapa adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Baada ya kupewa adhabu hiyo, Babu Seya na wanawe walikata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ambapo Jaji Thomas Mihayo (mstaafu), aliwatia hatiani na kuunga mkono hukumu ya Mahakama ya Kisutu, iliyotolewa na Hakimu Lyamuya.
Kutokana na hukumu ya Mahakama Kuu, Babu Seya na wanawe walikwenda Mahakama ya Rufaa, ambako Babu Seya na Papii Kocha walitiwa hatiani wakati Mbangu na Francis wakiachiwa huru.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Mahakama iliridhika na ushahidi ulio kwenye kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo kwa kila kosa na kwamba mrufani wa kwanza (Babu Seya) na wa pili (Papii Kocha), walihusika kutenda makosa. Ilisema  utetezi wao kwamba hawakuwa eneo la tukio ulikataliwa.
Katika hukumu hiyo,  Babu Seya alitiwa hatiani kwa makosa matano ya kunajisi na Papii Kocha makosa mawili.

No comments: