Thursday, October 31, 2013

CHADEMA YASISITIZA KWAO HAKUNA UKOMO WA MADARAKA...

Wafuasi na wanachama wa Chadema wakiandamana wakati wa moja ya mikutano ya chama hicho.
Chadema cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekiri kubadili kifungu cha ukomo wa uongozi kwa kutumia ilichoita utaratibu sahihi na haikuwa katika kutoa fursa kwa baadhi ya watu.

Kuondolewa kwa kifungu hicho, kunamfanya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kuwa na nafasi ya kugombea tena katika uchaguzi wa chama hicho mwakani na akipita, atakuwa mwenyekiti wa kwanza kuongoza kwa vipindi vitatu vya miaka mitano mitano.
Akizungumza katika makao makuu ya chama hicho jana, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaila ambaye pia alikuwa Katibu wa Kamati ya Maboresho ya katiba mwaka 2006, alisisitiza maboresho hayo yalifuata utaratibu.
Alisema mbali na kifungu hicho kuondolewa, pia mabadiliko hayo yalihusu kuongeza kifungu cha maadili na sifa za uongozi, ambayo yalikwenda sambamba na kuzindua upya chama hicho kikiwa na bendera mpya.
"Mabadiliko yalifuata taratibu zote, tunashangaa leo baada ya miaka saba ya mabadiliko huku uchaguzi wa pili ukitarajiwa kufanyika chini ya Katiba hiyo, anaibuka mtu kuhoji mabadiliko hayo.
"Kwa nini hakuweka pingamizi wakati ule, waliogombea aliwaona, anawafahamu, ni kwa nini hakuweka pingamizi mwaka 2009? Kwa nini leo? Ukijiuliza unaona kuna egemeo nyuma yake," alisema akimaanisha kauli ya Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba aliyesimamishwa uanachama.
Kigaila ambaye alisema mpaka sasa hakuna hatari yoyote kwa chama chake, na kuwa uamuzi wa kutoa ufafanuzi huo ni kutaka kueleza ukweli wa mambo kwa umma na wanachama wapya wa chama hicho ambao hawakuwapo wakati wa mchakato huo.
Hivi karibuni, Mwigamba alidai uongozi wa juu wa chama hicho umechakachua Katiba kwa kuondoa kipengele cha ukomo wa  madaraka ya uongozi kwa lengo la kubeba baadhi ya viongozi kuendelea kuongoza chama hicho.
Kuhusu kauli iliyodaiwa kutolewa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kuwa vikao vya majungu vimefanya wapigane, Kigaila alisema alihoji uelewa wa utendaji wa chama wa kiongozi huyo.
Alisema kikao cha Baraza la Kanda ya Kaskazini, kiliitishwa kihalali kutokana na utaratibu wa chama chake na kuwa wana haki ya kuendesha vikao na kuweka mikakati ya kikanda.
"Kama kweli kiongozi huyo alisema hayo, tunatakiwa tuhoji uelewa wake wa utendaji wa chama, mbona Zitto aliendesha kampeni Kanda ya Magharibi? Walifanya hivyo bila kupangiwa na makao makuu na baadaye kupeleka ripoti makao makuu."
Alisema kikao hicho kilijumuisha wajumbe wa Baraza Kuu, wabunge na viongozi wa mikoa kutoka Kanda husika na kuwa uwepo wa Mbowe ni kutokana na nafasi zake mbili kwenye kikao hicho, Mbunge wa Hai na Mwenyekiti.

No comments: